Mkongomani atua Coastal Union | Mwanaspoti

KLABU ya Coastal Union imekamilisha uhamisho wa beki wa kushoto raia wa Congo, Hernest Briyock Malonga kutokea Singida Black Stars kwa mkopo wa mwaka mmoja.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Habari na Mawasiliano wa Coastal Union, Abbas Elsabri amethibitisha timu hiyo kukamilisha uhamisho wa beki huyo, huku akiweka wazi ni mikakati kabambe ya msimu ujao.

“Msimu ujao tunashiriki michuano mingi kwa maana ya ndani na ile ya kimataifa hivyo kama timu ambayo tunataka kufanya vizuri ni lazima tupate wachezaji bora,” amesema na kuongeza;

“Usajili tulioufanya tumezingatia sana ripoti ya benchi letu la ufundi na kiukweli nikiri wazi tumepata wachezaji bora ambao tunaamini kabisa kadri wanavyozidi kuzoeana basi, timu yetu itakuwa ni tishio zaidi kwa msimu ujao.”

Malonga alisajiliwa na Singida kwa mara ya kwanza akitokea klabu ya Diables Noirs ya kwao Congo Brazzaville, huku akiwa mchezaji wa pili kujiunga na Coastal Union akitoka ndani ya kikosi hicho, baada ya awali ‘Wagosi wa Kaya’ kumtangaza beki wa kati, Mukrim Issa ‘Miranda’.

Related Posts