Naibu Waziri kushughulikia barabara Ubungo Maziwa, atembelea bandari kavu

Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile amesema ili uwekezaji wa Serikali katika miundombinu ilete matokeo chanya, changamoto zote zinazokwamisha ufanisi wa sekta binafsi zitapatiwa ufumbuzi.

Kihenzile amesema kero inayotokana na ubovu wa barabara ya kilomita moja katika eneo la bandari kavu Ubungo Maziwa, jijini Dar es Salaam inayoendeshwa na Kampuni ya Bravo Logistics, itatatuliwa.

Naibu Waziri huyo amesema hayo leo Jumatano Agosti 7, 2024, baada ya kufanya ziara ya kukagua utendaji wa bandari kavu eneo la Ubungo Maziwa pamoja na ile inayosimamiwa na Kampuni ya African Global Logistics, Dar es Salaam.

Ziara hiyo ni sehemu ya mpango wa kutafuta na kutatua kero za watoa huduma wanaodhibitiwa na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC).

“Zipo changamoto ambazo zimeelekezwa kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), hizo nitaawaagiza wahakikishe wanazifanyia kazi.

Suala la barabara, nitawasiliana na Wizara ya Ujenzi na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ili kuondoa kero hii kwa sababu sekta binafsi ni muhimu katika ukuaji wa uchumi,” amesema Kihenzile.

Naibu waziri huyo amesema mazingira yao yakiboreka, wigo wao wa kulipa kodi utaongezeka na uchumi  utazidi kukua.

Kihenzile amesema maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa viongozi hao ni kutatua kero zote zinazozuia maendeleo ya sekta binafsi katika shughuli zao za kila siku.

Maelekezo anayozungumza Kihenzile ni yale ya Julai 29, 2024, wakati Rais Samia akiongoza kikao cha Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), kuwaagiza wasaidizi wake wakiwamo mawaziri kukaa na sekta binafsi ili kutatua changamoto zao.

Msingi wa hoja hiyo ni malalamiko yaliyoibuliwa na sekta binafsi katika kikao hicho ambacho mwenyekiti wake ni Rais na hufanyika kila mwaka ambapo Rais Samia alisema baadhi ya changamoto zilizoibuliwa na sekta binafsi hazihitaji fedha kuzitatua bali ni uamuzi tu wa watendaji serikalini.

Kuhusu leseni kwa wawekezaji wa bandari kavu inayotolewa na TASAC, Kihenzile amesema kero kuu inayolalamikiwa ni leseni kuwa ya mwaka mmoja, wakati mapendekezo ya wawekezaji ni miaka mitano.

Sababu ya uhitaji wa leseni ya muda mrefu ni kuruhusu kampuni hizo kuandaa mipango ya muda mrefu na kuomba mikopo benki ili kuimarisha uwekezaji wao, jambo ambalo kwa sasa wanashindwa kufanya kutokana na kutokubalika kwa uwekezaji wao.

Kihenzile amesema leseni sasa inatolewa kwa miaka mitatu na hitaji la leseni ya miaka mitano litafanyiwa kazi, lengo likiwa ni kusaidia sekta binafsi kukuza uchumi wa Taifa kwa kiwango kikubwa.

“Serikali itaboresha mazingira kwa sababu hatuwezi kuboresha miundombinu ya barabara, reli na bandari bila kuangalia mfumo wa utoaji huduma. Lazima tuiangalie sekta binafsi,” amesisitiza.

Kwa upande wake, Msimamizi wa Uendeshaji Mizigo wa Kampuni ya Bravo Logistics, Bosco Haule amesema ubovu wa barabara ndio changamoto kubwa wanayokutana nayo kwa kuwa wakati wa mvua barabara haipitiki.

“Kwa siku tunapokea magari 50 hadi 100 yenye mzigo, lakini wakati wa mvua barabara haipitiki. Pia, tumeomba Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuondoa makontena ili kuongeza uwekezaji katika eneo la bandari kavu,” amesema.

Kwa upande mwingine, Kaimu Mkurugenzi wa TASAC, Nelson Mlali, amesema ziara hiyo ililenga kusikiliza changamoto za watoa huduma katika eneo la bandari na bandari kavu ambazo mamlaka hiyo inazisimamia kwa lengo la kuzitafutia ufumbuzi.

Related Posts