SURA MPYA…Safari hii mtaipenda Ngao ya Jamii 2024

WAKATI kesho ikiwa ni sikukuu ya wakulima nchini maarufu ‘Nanenane’, kutakuwa pia na burudani ya soka ambapo itapigwa michezo miwili ya nusu fainali ya Kombe la Ngao ya Jamii, kuashiria ufunguzi wa Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2024-2025.

Mchezo wa mapema saa 10:00 jioni utapigwa kwenye Uwanja wa New Amaan visiwani Zanzibar ambako Azam FC itacheza na Coastal Union huku saa 1:00 usiku ikipigwa mechi ya ‘Dabi ya Kariakoo’, kati ya Yanga na Simba kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Wakati michezo hiyo ikisubiriwa kwa hamu kujua ni timu zipi zitatinga fainali au zitakazocheza mshindi wa tatu Jumapili ya Agosti 11, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, Mwanaspoti linakuletea sura mpya kwa kila mmoja wao.

Kikosi hiki cha matajiri wa jiji la Dar es Salaam kama kinavyofahamika, tayari kimesajili nyota wapya tisa kwa msimu ujao, wakiundwa na Yoro Mamadou Diaby (Yeleen Olympique), Franck Tiesse (Stade Malien FC) na Ever Meza kutoka Leonnes FC.

Nyota wengine ni Jhonier Blanco (Aguilas Doradas), Adam Adam (Mashujaa FC), Nassor Saadun (Geita Gold), Mohamed Mustafa (Al-Merrikh), Cheickna Diakite (AS Real Bamako) na kiungo raia wa Mali, Mamadou Samake kutoka CR Belouizdad ya Algeria.

Licha ya uhodari na uwezo wa nyota hao, anayetazamwa zaidi ni mshambuliaji raia wa Colombia, Jhonier Blanco, kutokana na rekodi zake katika timu aliyotoka ya Aguilas Doradas ya mji wa Rionegro, inayoshiriki Ligi Kuu ya Colombia.

Blanco aliyezaliwa Oktoba 18, 2000, alianzia soka lake kwenye akademi ya Club Deportivo Estudiantil kabla ya kujiunga na timu ya Ligi Kuu ya Aguilas Doradas na baadaye akatolewa kwa mkopo kujiunga na kikosi cha daraja la kwanza cha Fortaleza CEIF.

Akiwa na Fortaleza CEIF aliyoichezea kwa mkopo msimu uliopita katika Ligi Daraja la Kwanza Colombia maarufu (Categoria Primera B) na kuiwezesha kupanda Ligi Kuu huku ikiwa mabingwa, alifunga jumla ya mabao 18 kwenye mechi 26 za mashindano yote.

Yanga ambao ni mabingwa mara tatu mfululizo wa Ligi Kuu Bara, wamejiimarisha pia kwa ajili ya mashindano mbalimbali msimu ujao ambapo wamenasa saini za nyota saba wakiongozwa na kiungo mshambuliaji Mzambia, Clatous Chota Chama kutokea Simba.

Nyota wengine ni Prince Dube (Azam FC), Chadrack Boka (FC Lupopo), Khomeiny Abubakar, Duke Abuya (Singida Black Stars), Aziz Andambwile (Fountain Gate FC) na mshambuliaji wa zamani wa Simba, Jean Baleke aliyetokea Al-Ittihad SCS Tripoli ya Libya.

Licha ya ubora wa wachezaji hao, mshambuliaji raia wa Zimbabwe, Prince Dube ameanza kuonyesha matumaini makubwa na kikosi hicho baada ya kufunga jumla ya mabao mawili katika michezo ya kirafiki ya maandalizi ya msimu (pre-season).

Dube alianza kufungua ukurasa wa mabao ndani ya timu hiyo wakati ilipopata mualiko wa kushiriki michuano ya Mpumalanga Premier International Cup 2024, iliyofanyika Afrika Kusini, ambapo Yanga ilishinda bao 1-0, dhidi ya wenyeji, TS Galaxy.

Nyota huyo akaendeleza moto wake wa mabao baada ya kufunga bao moja katika ushindi wa timu hiyo wa 4-0, dhidi ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, ikiwa ni sehemu pia ya kudumisha uhusiano wa kibiashara baina yao ulioanza tangu mwaka jana.

Ushindi huo haukuwa bure kwa Yanga kwani ilitwaa ubingwa wa michuano ya Toyota Cup 2024, iliyoandaliwa na timu hiyo, huku mbali na Dube aliyefunga wengine waliofunga pia ni Clement Mzize na mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita, Stephane Aziz Ki aliyepachika mabao mawili.

Timu hii inayofahamika kwa jina la utani la ‘Wagosi wa Kaya’ kutoka Tanga, imenasa saini ya nyota wapya wanane hadi sasa ambao imeshawatangaza, wakiongozwa na beki wa kati, Anguti Luis kutoka KCCA ya kwao Uganda na Abdallah Hassan (Bandari).

Nyota wengine ni Mbaraka Yusuph (Kagera Sugar), Ramadhan Mwenda (KCB), Haroub Mohamed Abdallah ‘Gattuso’ (Malindi), Mukrim Issa ‘Miranda’ (Singida Black Stars), Athuman Hassan Msekeni (Mlandege) na Gift Abubakar Ali kutokea (Proline).

Coastal iliyomaliza nafasi ya nne msimu uliopita katika Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 43, inaendelea kujiimarisha kwa ajili ya msimu ujao ambapo mbali na kushiriki michuano ya ndani itashiriki pia Kombe la Shirikisho Afrika.

Kikosi hicho kinachoshiriki michuano ya kimataifa kwa mara ya kwanza tangu mara ya mwisho kiliposhiriki mwaka 1989 na kuishia raundi ya kwanza, kitaanza kuchanga karata zake ugenini dhidi ya FC Bravos ya Angola kati ya Agosti 16 hadi 18.

Coastal imekuwa ya sita kukata tiketi ya CAF ikiwa nafasi ya nne baada ya KMC, Namungo, Biashara United, Geita Gold na Singida Fountain Gate, ambapo Tanzania Bara inatoa timu mbili zinazoshiriki Ligi ya Mabingwa na nyingine Kombe la Shirikisho.

Baada ya kukosa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa misimu mitatu mfululizo, Simba imeamua kufanya usajili mkubwa kwa ajili ya kuboresha kikosi hicho kwa msimu ujao, huku ikizingatia zaidi wachezaji wenye umri mdogo watakaoipambania timu hiyo.

Simba imeleta maingizo mapya 14, ambao ni Joshua Mutale aliyetokea Power Dynamos ya kwao Zambia, Steven Dese Mukwala (Asante Kotoko), Jean Charles Ahoua (Stella Club Adjame), Abdulrazack Mohamed Hamza (SuperSport United) na Valentino Mashaka (Geita Gold).

Wengine ni, Augustine Okejepha (Rivers United FC), Debora Fernandes Mavambo (Mutondo Stars FC), Omary Abdallah Omary (Mashujaa FC), Valentin Nouma (FC Saint Eloi Lupopo), Chamou Karaboue (Racing Club d’Abidjan), Yusuph Kagoma, Kelvin Kijili (Fountain Gate FC), Awesu Awesu (KMC FC) na kipa, Moussa Camara aliyesajiliwa kutokea Horoya AC ya Guinea.

Katika usajili huo, wapo wachezaji ambao wameonyesha matumaini makubwa kwa kikosi hicho wakiwemo winga, Joshua Mutale na kiungo, Debora Fernandes Mavambo ambao walionyesha kiwango kizuri katika kilele cha ‘Simba Day’, Agosti 3, mwaka huu.

Katika tamasha la ‘Simba Day’, Debora mwenye uraia pacha wa Congo Brazzaville ila anaichezea timu ya taifa ya Gabon, alifunga bao moja katika ushindi wa Simba wa mabao 2-0, dhidi ya APR FC ya Rwanda na kuvutia mashabiki wa kikosi hicho.

Related Posts