Aburutwa kortini kwa mashtaka saba ya kubaka, kulawiti wanafunzi watano

Bukoba. Mkazi wa Mtaa wa Kyamaizi, Kata ya Kahororo Manispaa ya Bukoba, Abdul Suleiman (30), amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya Bukoba akikabiliwa na kesi mbili za kuwabaka na kuwalawiti wanafunzi watano wa shule za msingi.

Kesi hizo zenye jumla ya mashtaka saba, zimesomwa jana Jumatano Agosti 14, 2024 mbele ya mahakimu wawili tofauti mahakamani hapo.

Kesi ya kwanza namba 22889/2024  imesikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi, Frola Kaijage na mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali, Everester Kimaro.

Akimsomea mashtaka, Wakili Kimaro alidai kuwa  kati ya Aprili na Julai, 2024, mshtakiwa alimbaka mwanafunzi wa darasa la tatu mwenye umri wa miaka tisa.

Mshtakiwa alikana tuhuma hizo, kesi imeahirishwa  hadi Agosti 28, 2024 itakapoanza kusikilizwa baada ya upelelezi kukamilika.

Katika kesi ya pili namba 22890/2024 yenye mashtaka sita, inadaiwa kwa nyakati tofauti aliwabaka na kuwalawiti wanafunzi wanne wenye umri kati ya miaka 7 hadi 9. Katika kesi hiyo, mashtaka ya kubaka ni manne na mawili ya kulawiti.

Kesi hiyo imesikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Endrew Kabuka na kuendeshwa na Wakili wa Serikali, Agness Awino.

Wakili Awino alidai mshtakiwa alitenda makosa hayo kati ya Aprili na Julai, 2024, tuhuma ambazo pia alizikana.

Kesi hiyo inaendelea kusikilizwa leo mahakamani hapo kwa mshtakiwa kusomewa hoja  za awali.

Related Posts