ASALI YA TANZANIA SASA KURUHUSIWA KUUZWA CHINA, WIZARA YATOA NENO

Na Mwandishi Wetu

SERIKALI ya Tanzania kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imesaini makubaliano ya kuruhusiwa kuuza asali yake nchini China huku ikisisitiza pia uwepo wa mikakati yenye lengo la kuongeza uzalishaji wa mazao yanayotokana na nyuki.

Akizungumza leo Agosti 15,2024 jijini Dar es Salaam katika hafla ya Tanzania na China wakisaini mkataba wa asali ya Tanzania kuruhusiwa kuuzwa katika nchi hiyo Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Dustan Kitandula amesema kutokana na uwepo na mwitikio wa sekta binafsi katika kuchangamkia fursa zilizopo kwenye sekta ya ufugaji nyuki, mwaka 2018 ,Tanzania ilianza mawasiliano na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kwa lengo la kufungua soko la asali la China.

“Mawasiliano hayo yamekamilika kwa mafanikio makubwa, ambapo leo hii tumesaini Itifaki ya kuuza asali ya Tanzania nchini China. Utiaji saini uliofanyika unaondoa kikwazo kilichokuwepo hapo awali na kukidhi haja ya wafanyabiashara wa Tanzania ya kuuza asali katika masoko ya China,”amesema Kitandula.

Ameongeza kufunguka kwa soko la asali nchini China kunaenda pamoja na kutekeleza masharti kadhaa yaliyobainishwa kwenye Itifaki.Moja ya sharti ambalo wafanyabiashara wenye nia ya kuuza asali nchini China, nchi za Umoja wa Ulaya na Marekani wanapaswa kutekeleza ni kuhakikisha kuwa Kampuni zao zinasajiliwa kwenye Mifumo ya Kimataifa ya Udhibiti wa Afya na Usalama wa Vyakula; Afya ya Mimiea; na Ulinzi wa Mazingira.

Aidha amesema usajili wa Wafanyabiashara/Makampuni katika mifumo hii hufanyika kwa njia ya kidigitali na Wizara yetu kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imeweka dawati maalum kwa ajili ya kusaidia Wafanyabiashara kujisajili.

Hata hivyo amesema hadi sasa ni kampuni 12 tu ndiyo yamejisajili kwenye mifumo hiyo , hivyo ametoa rai kwa kampuni ambayo bado hayajasajiliwa yawasiliane na Wizara ili yaweze kusajiliwa.

Pamoja na hayo amempongeza Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuhakikisha rasilimali zilizopo, ikiwemo misitu, nyuki na wanyamapori zinaendelea kuhifadhiwa kwa ajili ya matumizi ya sasa na vizazi vijavyo.

“Jitihada zake za uhifadhi wa rasilimali hizi, Rais Dk.Samia ameendelea kutangaza na kuvutia wawekezaji katika sekta yetu ya ufugaji nyuki. Uongozi wake umekuwa chachu ya kuimarika kwa Sekta ya Maliasili na Utalii, huku akilenga sio tu kutunza mazingira na bionuwai, bali pia kuboresha maisha ya Watanzania kupitia miradi mbalimbali.

“Ufugaji nyuki ni moja ya shughuli ya kiuchumi inayogusa moja kwa moja maisha ya wananchi wa kawaida hususan wale wanaoishi karibu na maeneo yaliyohifadhiwa. Shughuli hiyo imekuwa ni chanzo muhimu cha ajira, hasa kwa vijana na wanawake, ambapo takribani watu milioni mbili nchini wamejiajiri kupitia ufugaji nyuki,”amesema.

Pia amesema Tanzania ina maeneo makubwa ya misitu yenye ukubwa wa takribani hekta milioni 48.1, ambapo ufugaji nyuki hufanyika kwa kiwango kikubwa.

Hivyo amesema kutokana na uwepo wa misitu hiyo, inakadiriwa Tanzania ina uwezo wa kuzalisha takribani tani 138,000 za asali kwa mwaka. Hata hivyo, kwa sasa uzalishaji wa asali upo kwenye kiwango cha takribani tani 33,276 sawa na asilimia 24.1 ya uwezo uliopo.

“Kiwango hiki kinaiweka Tanzania katika ramani ya Dunia na kuifanya kuwa nchi ya kwanza kwa uzalishaji wa asali katika nchi za Afrika Mashariki na SADC; nchi ya Pili kwa uzalisahji wa asali barani Afrika; na nchi ya 14 Duniani kwa uzalisahji wa asali.

“Hii inaonyesha sekta ya ufugaji nyuki ni muhimu kwa uchumi wa Tanzania na ina nafasi kubwa ya kuendelea kukua na kuchangia zaidi katika Pato la Taifa na ajira kwa wananchi.Pamoja na kiwango hiki cha uzalishaji asali, ni asilimia tano ya asali yote inayozalishwa ndiyo inauzwa katika masoko ya nje ya nchi.”

Ameongeza kiwango hiko kimechangiwa na sababu mbalimbali ikiwemo masharti mbalimbali ya kibiashara yaliyowekwa na nchi zinazonunua asali na kwamba asali ya Tanzania huuzwa hasa nchi za Umoja wa nchi za Ulaya kama Ujerumani, Poland, Denmark, Uholanzi, nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu, Uingereza, Marekani, Lebanon, Ubelgiji, Iraq, Saud Arabia, Kenya, Rwanda, Burundi, Congo na Uganda.

Aidha, wastani wa tani 793.5 za nta inayozalishwa nchini huuzwa katika masoko ya Japan, Amerika, Poland na Ujerumani. Mauzo hayo ya Asali na Nta nje ya nchi huipatia Tanzania wastani wa Dola za Kimarekani milioni 12.9 sawa na shilingi bilioni 30.58 kwa mwaka.

Kitandula amesema kutambua fursa kubwa ya biashara ya asali na mazao mengine ya nyuki, Serikali imeweka mikakati madhubuti ili kuongeza kiwango cha uzalishaji na ubora wa asali pamoja na kuongeza mauzo ya asali na mazao mengine ya nyuki nje ya nchi.

Amesema moja ya mikakati hiyo ni kuweka mazingira rafiki kwa soko la Asali katika nchi za Umoja wa Ulaya na Uingereza, kwa kuweka na kusimamia utekelezaji wa Mpango wa Udhibiti wa Mabaki ya Kemikali katika Asali.

“Mpango huu unalenga kuhakikisha asali inayozalishwa nchini inakidhi viwango vya ubora vinavyohitajika na masoko ya kitaifa, kikanda na kimataifa.Pia Serikali imeweka mfumo wa ufuatiliaji wa ubora wa asali unaojulikana.Mfumo huu unatumika kutunza na kutoa taarifa za wazalishaji na wafanyabiashara wa mazao ya nyuki,”amesema.

Kwa upande wake Waziri na Katibu wa Kamati ya CPC ya Utawala Mkuu wa Forodha ya Watu, Jamhuri ya China Yu Jianhua amesema mkakati wa China ni kuwa karibu na Tanzania kutokana na urafiki wa kimkakati wa miaka mingi baina ya nchi mbili hizo.

“Hiki kilichotokea leo ni mwendelezo wa historia ya miaka mingi ya uhusiano baina ya China na Tanzania, tumeingia makubaliano ya itifaki kununua asali kutoka Tanzania, lakini ninaamini kuna mengi zaidi tutayafanyaa,” amesema.

Amebainisha China ina soko la zaidi ya watu bilioni 1.4, kila mwaka wanaagiza asali kiasi cha zaidi ya tani milioni 38, hivyo wanaamini fedha nyingi zitaingia katika uchumi wa Tanzania kupitia biashara hiyo.