‘Bidhaa asili zifuate mfumo wa mauzo ya kahawa kuongeza ufanisi’

Dar es Salaam. Mfumo wa mauzo ya zao la kahawa umetajwa kuchagiza zao hilo kuongoza kwenye uuzaji wa bidhaa asilia nje ya nchi kwa miaka mitano mfululizo kuanzia 2019- 2023.

Takwimu za Msingi Tanzania zinazotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imeonyesha, zao la kahawa mauzo yake nje yamekuwa yakiongezeka kutoka Sh349.4 bilioni mwaka 2019  hadi Sh542.6 bilioni mwaka 2023.

Zao hilo ndilo linaloongoza likifuatiwa na pamba ambayo mauzo yake mwaka 2019 yalipanda kutoka  Sh212.3 bilioni hadi kufikia Sh245.9 bilioni, chai ikishika nafasi ya nne baada ya katani ambayo  mauzo yalikuwa ni Sh104 bilioni na kushuka kufikia Sh73.3 bilioni.

Meneja wa Ubora wa Mauzo ya Kahawa, Frank Nyarusi amesema njia iliyochangia kahawa kutawala mauzo soko la nje ni kutumia mifumo mitatu kwenye mauzo.

Amesema wanaanza na soko la awali ambalo wakulima hupitia vyama vya ushirika kuuza kahawa aina ya Arabika na Robusta.

“Rubosta huuzwa kwa mnada mkoani Kagera kupitia chama cha ushirika, kahawa huuzwa kwa pamoja anayenunua ananunua kahawa yote ya chama, hii tunafanya kwa njia ya mtandao.”

Njia hii imeongeza zaidi idadi ya wanunuzi kwa sababu si lazima mtu asafiri kwenda Kagera kwa ajili ya kushiriki mnada,” amesema.

Nyarusi amesema kupitia mfumo huo watu hushindana bei mtandaoni kupitia mataifa mbalimbali kununua zao hilo.

Njia ya pili ameitaja ni uongezaji wa thamani wa zao hilo ikihusisha uuzwaji wa kahawa safi.

“Njia hii mkulima huiongezea thamani kahawa na kuiweka kwenye madaraja na kuiuza akiwa ameiongezea ubora,” amesema.

Utaratibu mwingine wa mauzo ni uhusiano wa moja kwa moja kati ya mfanyabiashara na mkulima kuuziana kahawa kupitia chama cha ushirika kokote alipo.

“Mkulima anakuwa na uhusiano na mkaangaji wa kahawa Japan au Ulaya anakuwa anamuuzia moja kwa moja na utaratibu huo unaleta uhusiano wa moja kwa moja na unaongeza mtaji na uhakika wa soko kwa mkulima,” amesema.

Njia hiyo amesema husaidia wakulima na wafanyabiashara kuingia makubaliano ya muda mrefu ya namna ya kuzalisha kahawa bora na bodi hiyo ndio huidhinisha mkataba huo.

Kila jambo linalofanyika kwenye kilimo cha kahawa, Meneja huyo amesema wanahakikisha wanaangalia masilahi ya mkulima na mfanyabiashara.

Kwa takwimu za NBS, mwaka 2019 kahawa iliyouzwa ilikuwa Sh349.4  bilioni mwaka 2020  ikauzwa Sh331.5 bilioni, mwaka 2021 Sh354.8 bilioni na mwaka 2022 ni Sh369.4 bilioni na  2023 Sh542.6 bilioni.

Kwa zao la pamba NBS imeonyesha, mwaka 2019 mauzo ya zao hilo nje ya nchi ilikuwa Sh212.3 bilioni na 2020 ikafikia Sh199.8 bilioni na mwaka 2021 Sh185.9 bilioni, mwaka 2022 ukafikia Sh237.1 bilioni na mwaka 2023 ikapanda kufikia Sh245.9 bilioni.

Utofauti wa mauzo hayo pia upo kwenye mfumo wa mauzo, Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba Marco Mtunga anaeleza njia inayotumika kwenye mauzo ya pamba kuanzia mwaka 1992.

Amesema tangu mwaka huo Serikali iliruhusu kampuni binafsi kufanya biashara na kuondoa vyama vya ushirika kufanya biashara hiyo pekee.

“Tuna kampuni zaidi ya 27 ambazo zinanunua pamba kwa wakulima, mfumo tunaoutumia vijijini ni vyama vya msingi vya ushirika Amcos ambavyo vinakuwa kama mawakala.”

“Wanunuzi huweka bei yao na fedha, mkulima akienda kufanya mauzo anachagua kampuni yenye bei nzuri,” amesema.

Mtunga amesema baada ya kampuni hizo kununua pamba kila moja huchukua pamba yake na kupeleka kiwandani, akisisitiza  idadi ya kampuni zinazofanya biashara nje ni nyingi.

Kuhusu bei, amesema kabla ya kuanza msimu mwingine mauzo, Wizara ya Kilimo, Bodi ya Pamba, wanunuzi na wawakilishi wa wakulima hupitia vigezo vyote na kukubaliana bei ya kuanzia sokoni kulingana na bei ya soko la dunia, mabadiliko ya fedha za kigeni na bei ya mbegu ndipo hukubaliana.

Amesema mwanzoni mwa mwaka huu walianza na bei ya Sh1,150 lakini sasa pamba huuzwa hadi Sh1,600.

Kwa zao la chai, takwimu za NBS zinaonyesha mwaka 2019 mauzo yalikuwa Sh104.0 bilioni, mwaka 2020 ikafikia Sh74.0 bilioni mwaka 2021 ikafikia Sh75.2 bilioni na 2022 Sh68.8 bilioni na Sh73.3 bilioni zilipatikana mwaka 2023.

Mfumo wa mauzo ya zao hilo unafafanuliwa na Ofisa Mawasiliano Bodi ya Chai Tanzania, Evance Ng’ingo akisema chai huuzwa kwa mfumo wa Tehama kupitia ATMIS inayomsaidia muuzaji kupata bei kwa njia ya mtandao.

“Pia wafanyabiashara wanawafuata wakulima kununua chai, pia kupitia ushirika mnada unaendeshwa na mtu wa bei kubwa anauziwa,”amesema.

Amesema ya zao hilo nje ya nchi, wafanyabiashara hujisajili kidijitali na kupewa kibali cha kusafirisha nje ya nchi.