Bunge kuendelea kutunga sera za kunufaisha wajasiriamali

Dar es Salaam. Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania limeahidi kuendelea kutunga sheria na sera zitakazoweka mazingira bora ya maendeleo ya wajasiriamali.

Hayo yamesemwa leo Agosti 15, 2024 ma Spika wa Bunge hilo, Dk Tulia Ackson alipotembelewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara Tanzania (TCB), Adam Mihayo ofisini kwake jijini Dodoma.

Dk Tulia amesisitiza wajibu wa Bunge katika kutunga sera zinazowezesha maendeleo ya wajasiriamali na kuhakikisha kwamba biashara zao zinapata rasilimali zinazohitajika ili kukua.

 “Maendeleo ya wajasiriamali ni muhimu kwa ukuaji uchumi wa Taifa letu, kupitia ushirikiano huu na Benki ya TCB, tunaweza kutengeneza mazingira yatakayowezesha ukuaji wa biashara,“ amesema.

Mihayo aliambatana na Mkurugenzi wa Biashara za Wateja Wadogo na wa Kati wa benki hiyo, Lilian Mtali, katika ziara hiyo ambayo inafungua ukurasa mpya wa ushirikiano baina ya Benki ya TCB na Bunge la Tanzania katika kuwainua wajasiriamali wadogo na wa kati nchini.

Wakitambua mchango wa kundi hili katika ukuaji uchumi na uzalishaji wa ajira mpya, mazungumzo yao yamejikita katika kuanzisha mpango wa ruzuku, mikopo ya riba nafuu, na misamaha ya kodi kwa wajasiriamali.

Miradi hii itasaidia kukuza na kuchochea mazingira ya biashara kwa wajasiriamali pamoja na biashara zao.

“Lengo letu sio kutoa jibu moja kwa nchi nzima. Huwezi kuwa na suluhisho moja kwa watu wote, ndiyo maana ni muhimu kuwasikiliza wadau wengi iwezekanavyo. Njia hii itatusaidia kutoa majibu yatakayokidhi mahitaji ya wajasiriamali kulingana maeneo wanayoishi hata wale walioko vijijini,” amesema Mihayo.