WAKATI pazia la Ligi Kuu Bara msimu wa 2024-2025 likitarajiwa kuzinduliwa rasmi kesho Ijumaa kwa kupigwa mechi moja kati ya Pamba Jiji na Tanzania Prisons, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha ambaye ni mlezi wa Tabora United amewatuliza presha mashabiki wa timu hiyo akisema wamejipanga vilivyo kufanya vyema msimu huu tofauti na uliopita walipokaribia kushuka daraja.
Tabora iliyokuwa imefungiwa kusajili kutokana na kushtakiwa Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) kabla ya kufunguliwa jana Jumatano ikiwa ni saa chache kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili usiku wa leo Alhamisi, jambo lililowatia hofu mashabiki wakiamini huenda chama lao likayumba kama msimu uliopita.
Hata hivyo, akizungumza na Mwanaspoti, RC Chacha amesema licha ya kufungiwa usajili, lakini klabu haikukaa kizembe na badala yake iliendelea na yake na imefanya usajili wa kutisha na wa kuwababe msimu huu.
“Hadi tunafunguliwa kusajili kuna kazi kubwa tumeifanya, licha ya ukimya wetu tumefanikiwa kusajili kwa kiasi kikubwa, tumeimarisha kila eneo zaidi ya msimu uliopita na tunatarajia kuonyesha ushindani katika msimu huu,” amesema Chacha.
Chacha amesema katika mchezo wa kwana wa kufungua msimu dhidi ya Simba utakaopigwa keshokutwa Jumapili, timu hiyo imepanga kupambana kuonyesha ubora na kwamba hategemei kuanza na wachezaji pungufu kama ilivyotokea msimu uliopita ilipocheza kwa mara ya kwanza Ligi Kuu ikianza na Azam FC.
Katika mechi hiyo ya msimu uliopita uliopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es Salaam Tabora ilianza na wachezaji nane kabla ya baadae wawilui kujivunja na kulifanya pambano limalizike likiwa limecheza dakika zisizozidi 25 ikiwa imeshafumuliwa mabao 4-1, kisha kuupoteza mchezo huo kwa maamuzi ya Kamati ya Kuendesha na Kusimamia Ligi.
“Ni kweli hatujacheza mechi za kirafiki kwa kuonekana, na watu wengi hawajui kikosi chetu lakini kuelekea mchezo wa Simba, kwa maandalizi tuliyofanya mashabiki wakiunge mkono kikosi chao wakiamini kwamba msimu huu kitakua tofauti na msimu uliopita,” amesema Mkuu wa Mkoa huyo.
Kwa upande wa George Isaya, shabiki wa Tabora Utd amesema kwa vile ligi inaanza kesho anaomba mapema timu hiyo isiwape presha mashabiki kwa kufanya vibaya.
“Tumeambiwa timu imefichwa na imesajili vizuri , siku zote soka halijifichi tunaamini timu itafanya vizuri na kwa msimu ujao hatutaku kuwa na presha kama msimu uliomalizika maana tunataka burudani kutoka kwa timu yetu,” amesema shabiki huyo.
Tabora ilisalia katika Ligi ya msimu huu baada ya kushinda mechi za play-off dhidi ya Biashara United ya Ligi ya Championiship kwa jumla wa mabao 2-1, Wanajeshi wa Mpakani wakishinda mjini Musoma kwa bao 1-0 kabla ya Nyuki kupindua meza kwa mabao 2-0 ziliporudiana kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi.