Mwanafunzi asimulia dakika za mwisho mwenzao aliyefia mazoezini

Moshi. Zikiwa zimepita siku tatu tangu kutokea kifo cha mwanafunzi wa kidato cha tano katika Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Umbwe, iliyopo Wilaya ya Moshi, Thomas Kogal (19), mwanafunzi mwenzake, Mohamed Rajab amesimulia alivyozungumza naye dakika za mwisho kabla ya mauti kumfika.

Thomas aliyekuwa anasoma mchepuo wa sanaa (HKL), alifariki dunia Jumatatu Agosti 12, 2024 shuleni hapo akiwa mazoezini na wenzake wa chama cha skauti baada ya kujisikia vibaya.

Mwili wake leo Alhamisi Agosti 15, 2024   unasafirishwa kuelekea nyumbani kwao mkoani Kigoma kwa maziko.

Akizungumza na Mwananchi baada ya kuaga mwili, mwanafunzi Mohamed ambaye ni miongoni mwa waliyekuwa naye wakati wanafanya mazoezi hayo, anasema mazoezi hayo ni ya kujiandaa na maonyesho ya Skauti kuelekea maadhimisho ya miaka 75 tangu kuanzishwa kwa shule hiyo.

Mohammed anayesoma kidato cha sita shuleni hapo anasema baada ya uongozi wa shule hiyo kutangaza maadhimisho ya jubilee ya miaka 75 ya shule hiyo, wanafunzi ambao ni wanachama wa chama hicho walianza maandalizi ambayo ni pamoja na kufanya mazoezi.

Thomas alikuwa mwanachama, lakini hakuwahi kuja mazoezini ila baada ya kutangazwa maadhimisho hayo alianza kushiriki mazoezi.

“Alijiunga na skauti na hakuwahi kuja mazoezini ila baada ya kutangazwa tukio la jubilee ya miaka 75 ya Umbwe, skauti kama kikundi kimojawapo tuliambiana kila mwananchama anapaswa kushiriki mazoezi ili siku ya kilele tuonyeshe onyesho letu siku ya jubilee,” amesimulia mwanafunzi huyo na kuongeza;

“Jumatatu (Agosti 12) tukiwa mazoezini huwa tuna utaratibu wa kufanya mazoezi ya kuchangamsha mwili kwa kukimbia sasa wakati tunakimbia, akaishiwa nguvu.”

Mohammed anasema Thomas aliwaambia anajisikia kuchoka na haukupita muda akadondoka chini.

Anasema walitoa taarifa kwa mwalimu wao  ambaye haraka alifika eneo walilokuwepo na kumpatia huduma ya kwanza na baadaye wakampeleka Kituo cha Afya Umbwe.

“Neno la mwisho alituambia anajisikia kuchoka na anaishiwa nguvu, alivyosema vile hazikupita hata sekunde kadhaa akaanguka chini.Tulijitahidi kumpa huduma ya kwanza na mwalimu alipofika muda mfupi tukamchukua na kumpeleka Kituo cha afya cha Umbwe, hapo ndipo tukaambiwa amekufa,” amesimulia mwanafunzi huyo.

Mohammed anasema wamepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha mwanafunzi mwenzao ambacho kimetokea ghafla huku akiwa mazoezini.

“Tunamwombea kwa Mungu apumzike salama, ila tumeumia sana na hatujui ni ugonjwa gani umemuua mwenzetu,” amesema mwananfunzi huyo.

Hata hivyo, taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa inasema kifo cha Thomas kimesababishwa na  mshtuko wa moyo.

“Taarifa ya awali tuliyopatiwa na daktari inasema mwanafunzi huyu alipata mshituko wa moyo akiwa mazoezini ndiyo uliosababisha kifo chake,” amesema Kamanda Maigwa.

Akizungumzia kifo hicho, Mratibu wa Skauti Wilaya ya Moshi, Rashid Rashid amesema kifo cha mwanafunzi huyo ni pigo kubwa kwa wanachama hao na kwamba, watamkumbuka kwa mengi.

“Tumepokea kwa masikitiko makubwa msiba wa mwenzetu Thomas ambaye ni mwanaskauti mwenzetu, kifo chake kimetuumiza sana, hivyo leo tumekuja kuungana naye katika safari yake ya mwisho na ndio maana skauti tupo hapa wa kutosha kuhakikisha tunamsindikiza mwenzetu katika safari yake ya mwisho,” amesema Rashid.

Akizungumza kwa niaba ya Mthibiti Ubora wa Elimu Kanda ya Kaskazini Mashariki, Amon Mrutu,  amesema kifo hicho ni pigo kubwa kwa wazazi, walimu na wanafunzi wenzake kwa kukuwa hakikutarajiwa.

“Tumepokea kwa masikitiko makubwa msiba wa huyu mtoto wetu, mwanafunzi wetu ambaye tumempokea siku chache tu hapa shuleni, lakini siri ya Mungu dhidi ya maisha yetu ni nzito sana, sisi tunaweza tukawa tumempenda lakini Mungu akawa amempenda zaidi hivyo tuendelee kumuombea,” amesema Mrutu.

Akizungumza na Mwananchi jana Jumatano Agosti 14, 2024, Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Umbwe, Danloard Nyimbi alisema mwanafunzi huyo (19) alifikishwa hospitalini hapo tayari akiwa ameshafariki dunia.

Alisema wanafunzi waliomfikisha hospitalini hapo walidai kuwa wakati wanafanya mazoezi,  mwenzao huyo aliwaambia anajisikia kuchoka na baadaye aliendelea na mazoezi na ghafla alidondoka chini.

“Wanasema eneo walilokuwa wanafanya mazoezi kuna kamlima kidogo alikuwa anapandisha, wenzake walienda kama mizunguko 10 hivi, yeye alipoenda mzunguko wa kwanza akadai amechoka, wakamuuliza nini shida akawajibu huwa anakula pilipili nyingi,”alisema.