Rais Samia awataka wateule kujiongeza, Jaji Mkuu atia neno

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi aliowateua kwenda kufanya kazi kwa kutumia umahiri wa taaluma walizosomea na panapotakiwa kujiongeza wafanye hivyo.

Mkuu huyo wa nchi, aliyetumia chini ya dakika tatu kutoa neno kwa wateule aliowaapisha, ameahidi kuwaita viongozi hao kila sekta kwa ajili ya kuzungumza nao.

Rais Samia ameyasema hayo leo, Alhamisi Agosti 15, 2024 baada ya kuwaapisha wateule aliowateua jana Agosti 14.

“Ninachotaka kusema ni kile alichokisema Makamu wa Rais kuwa kwenye kufanya kazi zenu kuna umahiri wa ulichosomea na kujiongeza kutumia ‘common sense’. Pale unapoona ‘common sense’ inaweza kutumika vizuri tumieni, jiongeze, fanyeni kazi tuwatumikie wananchi,” amesema Samia.

Kutokana na safari aliyokuwa nayo leo ya kuhudhuria vikao vya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), amesema atazungumza na wateule hao kwa sekta zao kwa kadri itakavyopangwa.

Hata hivyo, ameeleza mabadiliko aliyoyafanya ni ya kawaida yanayolenga kuongeza ufanisi katika utendaji.

“Tunachotarajia kwenu ni kuongeza ufanisi katika maeneo yenu. Mmeapa hapa kiapo cha maadili na kiapo kwa dini zenu mnazoamini, mkaishi na viapo hivyo lakini pia mkafuate maadili ya kikazi yanayotakiwa,” amesema Rais Samia.

Profesa Juma: Tatizo sio sheria ni wanaopewa nafasi

Akizungumza katika hafla hiyo, Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma amesema mapungufu ya sheria, bajeti au taasisi si changamoto zinazozikabili nchi zinazoendelea, bali tatizo ni wanaopewa nafasi za kutekeleza sheria na wale wanaolengwa nazo.

Kwa mujibu wa Profesa Juma, matatizo kwa wanaopewa nafasi hizo yanatokana na wengi wao kuwa na tabia na tamaduni binafsi ambazo hupoteza malengo yanayolengwa na sheria.

“Kwa hiyo tunapokwenda sehemu zetu za kazi, pamoja na kuangalia sheria lakini lazima tuangalie nafsi zetu wenyewe, tuna fikra hasi zozote, tuna tabia ambazo zinafanya sheria zisifanye kazi,” amesema.

Sambamba na hilo, Jaji Mkuu huyo amesema ni muhimu jamii isiweke msisitizo zaidi katika kudai haki, bila kutimiza wajibu wanaopaswa.

“Watu wengi wameshajitokeza kwamba sasa hivi tunatawaliwa zaidi na haki lakini tunasahau kwamba demokrasia inajengwa zaidi na kuwajibika, wewe mwenyewe mwananchi unayelengwa na sheria una wajibu kwa nchi yako je, tunatimiza hilo sharti kwa namna gani,” amesema.

Amewataka wateule wote kulinda imani waliyopewa na Rais Samia, akisema kinyume na kufanya hivyo wataipoteza imani hiyo.

Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amewataka wateule wote kuviishi viapo walivyokula na kutimiza matumaini ya Rais Samia ya kuona Watanzania wanapata huduma bora.

“Kila mmoja akafanye kazi kwa bidii mkashirikiane na viongozi wengine mtakaowakuta kwenye nafasi zao ili twende sawa kama Taifa,” amesema.