Dar es Salaam. Kituo cha daladala katika Soko la Machinga Complex kilichopo, Wilaya ya Ilala kimezidiwa na idadi kubwa ya daladala hali iliyosababisha Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini(Latra) kusitisha utoaji vibali wa ruti zinazoishia kituoni hapo.
Kabla ya soko hilo kuchanganya kibiashara, malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara ilikuwa ni daladala kutopita hapo kushusha abiria ambao wangeweza kufanya ununuzi.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumamosi Agosti 17 2014, Ofisa Mfawidhi wa Latra Mkoa wa Dar es Salaam, Rahim Kondo, amesema katika kituo hicho kuna ruti zisizopungua tano, lakini kutokana na udogo wa kituo, kuna wakati gari hizo zinaegeshwa nje.
“Nadhani kuna haja Halmashauri ya Ilala kuona namna gani inaweza kutenga eneo lingine ili magari yaweze kufika, kwa kuwa ukweli ni kwamba kuna uhitaji wa usafiri wa abiria kufika hapo,” amesema Rahimu.
Akilizungumzia hilo, Ofisa Uhusiano wa Jiji la Dar es Salaam, Tabu Shaibu, amesema kwa kuwa Latra ndio waongoza magari, ni vema wakawaandikia barua kupendekeza ni wapi wanaona panafaa kuwa na stendi karibu na maeneo hayo.
“Hadi sasa suala hilo halijafika mezani kwetu, lakini Latra wanaweza kutuandikia barua kupendekeza ni wapi wanaona panafaa kwa kuwa malengo yetu ni kuwarahisishia wananchi kupata usafiri,” amesema Tabu.
Mwenyekiti wa Chama cha Madereva wa Daladala za Kigamboni – Machinga Complex, Hamis Said, amesema gari za Kigamboni na Vijibweni, ndio zipo nyingi katika kituo hicho ukilinganisha na za ruti nyingine huku akieleza sababu ni kutokana na ruti hiyo kuwa fupi watu wameonekana kuichangamkia.
“Hapa tuna gari zinazotoka Kigamboni, Vijibweni, Chanika, Homboza, Kijiwe Samli na Kitunda, yaani gari zote kwenye stendi hii zinaweza kufika 90, lakini uwezo wa kituo ni kubeba daladala sio zaidi ya 50 na bado hapo kuna watu wanataka kuleta magari yao hapa, hivyo sisi viongozi tayari tumelifikisha hilo Latra kuona namna gani wanaweza kufanya,” amesema Said.
Hata hivyo, amependekeza kuwa eneo la wazi nyuma ya vibanda vya walemavu Soko la Mchikichini kunaweza kufaa kuwa stendi pindi wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo waliowekwa pale kwa muda watakapoondoka.
Ally Said dereva wa daladala za Chanika – Machinga Complex, amesema anachoshukuru wao njia yao abiria ni wengi hivyo hawakai sana stendi na kubainisha kuwa kuna ukweli kuwa kituo hicho kimezidiwa kwa kuwa hata daladala za Kigamboni kuna wakati zinakaa kwenye mstari wao.
Wakizungumzia hali hiyo baadhi ya wafanyabiashara, Chikoa Andrew, amesema tangu kuhamia kwa wafanyabiashara kutoka Soko Kariakoo, biashara eneo hilo imechangamka na hivyo kuwavutia wengi kwenda kufanya ununuzi hapo.
Baadhi ya abiria wakilizungumzia hilo, Ndole Chacha, mkazi wa Kigamboni, amesema kuna haja ya kituo hicho kutanuliwa kwa kuwa ruti hiyo ni mwokozi wa abiria wanaotoka pembezoni mwa mji kwenda Kariakoo.
Idrisa Kimweru mkazi wa Kijiwe Samli, amesema haoni kama kuna haja ya kuwepo kwa uwanja wa mpira eneo lile, alipendekeza pangejengwa stendi kubwa pale ingeweza kupunguza adha hiyo ya msongamano wa daladala unaokua zaidi saa ambazo hamna abiria wengi.