LICHA ya mipango mizuri ya kutaka kuona Ligi ya Kikapu Mkoa wa Kigoma inaanza na kumalizika mapema, mambo yameenda sivyo kutokana na klabu shiriki kushindwa kukamilisha utaratibu wa kujisajili ikiwemo kulipa ada ya Sh100,000.
Ligi hiyo ilipangwa kuanza Agosti 8, lakini hadi sasa imeshindwa kuchezwa na uongozi wa kikapu mkoani humo umeeleza sababu, japo unapambana ili ianze mapema.
Katibu Mkuu wa Chama cha Kikapu Mkoa wa Kigoma, Aq Qassim Anasi ameliambia Mwanaspoti kuwa, ligi hiyo imekwama kuanza kama ilivyopangwa kutokana na timu shiriki kuikwamisha kwa kushindwa kulipa ada ya ushiriki ya Sh100,000 inayolipwa na kila timu ambazo hutumika pia katika uendeshaji wake.
Anasi alisema klabu tano ndizo zilizothibitisha kushiriki ligi hiyo ambazo ni; Tanganyika BC, Lake Side, Spide, Kasulu na Kibondo.
Katibu huyo ambaye pia ni kocha wa timu ya Mkoa wa Kigoma na ya taifa ya vijana U16, alisema fedha hizo za ada ndizo ambazo hutumika pia kuwalipia marefa wa ligi hiyo, hivyo kwa klabu kushindwa kulipa imefanya ligi isianze kwani wanahofia kukwama njiani.
“Hadi sasa tunapambana timu zilipe ada ya ushiriki na huku tukitafuta wadhamini wa kuipiga tafu ligi hiyo ya mkoa na tunatoa wito kwa wadau wa mchezo huo mkoani hapa kutusaidia,” alisema Anasi.