Arusha. Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, amewaonya wataalamu na watendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Arusha (AUWSA) na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa), wenye tabia ya kuchukua rushwa kwa baadhi ya makandarasi na kusababisha miradi kutekelezwa chini ya kiwango.
Makonda amesema mkoa utakutana na Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso kujadili gharama kubwa za uendeshaji mradi wa maji unaotekelezwa katika Jiji la Arusha wa Sh520 bilioni.
Amesema hayo leo Agosti 17, 2024 kwenye kikao kazi cha kujadili hali ya upatikanaji wa maji na namna ya kukabiliana na changamoto za upatikanaji wa maji, ikiwamo mabadiliko ya tabianchi.
Makonda amesema ni muhimu watendaji na wataalamu kufanya kazi kwa weledi na kujiepusha na rushwa ili miradi ikamilike na wananchi wapate maji.
“Jiepusheni na rushwa, hawa watu wanaojenga miradi hii, mfano tumekubaliana tunataka tuchimbe kisima chenye urefu wa mita 150 ninyi ndiyo mnaosimamia, badala ya 150 anachimba mita 50 yatapatikana maji, viongozi watafurahia maji yametoka kumbe ninyi mnajua hajaenda mita 150,” amesema Makonda.
“Kwenye malipo amelipwa gharama ya kuchimba mita 150, matokeo yake tukiingia kwenye kiangazi au mabadiliko ya tabianchi maji yanaisha, naomba tuwe waadilifu. Nitatengeneza timu kupita kwenye miradi yote kukagua kwa sababu tunashindwa kuwa waadilifu, tusifurahie mradi unaoonekana umekamilika baada ya muda maji hayatoki,” amesema.
Makonda amesema miradi imekuwa ikitumia fedha nyingi, hivyo lazima waongeze umakini kwenye usimamizi kuanzia wakati wa usanifu ili ilete matokeo chanya.
Amesema licha ya kutekelezwa miradi mbalimbali ikiwamo mikubwa, wananchi wanaishi kwa mgawo kwa maji.
Amezungumzia mradi huo mkubwa wa maji wa Sh520 bilioni uliotekelezwa jijini Arusha ambao umetajwa kukamilika na kutoa maji lita milioni 200 kwa siku, lakini usanifu ulikosewa.
Makonda amesema licha ya mradi huo kukamilika bado kuna changamoto hivyo ili kuitatua watakutana katika kikao.
“Lazima tukutane ili tutafute ufumbuzi wa haraka Wizara ya Nishati ituingize kwenye watoa huduma wa makazi badala ya viwandani ili kupunguza mzigo wa kuendesha mradi huu,” amesema.
Makonda amesema kuanzia usanifu wa mradi huo ulikosewa, hivyo AUWSA walipaswa kuuza uniti moja ya maji kwa wananchi Sh3,400 ila wanauza uniti moja Sh1,800, na kutokana na gharama za kuendesha mitambo ya kutoa maji kuwa kubwa inakuwa mzigo kwa mamlaka hiyo.
“Serikali imeshindwa kutoza uniti moja Sh3,400 hivyo wananchi wanauziwa uniti moja Sh1,800, nani analipia Sh1,600 inayobaki? Ndiyo maana mkiwasha pampu zote gharama ni kubwa, kwa hiyo gharama za kuendesha mradi huu ni kubwa na hatuwezi kukubali wananchi waongezewe bei, hivyo tutakaa kuomba Tanesco wapunguze bei ya kuendesha mradi ili wananchi wapate maji,” amesema.
Mkurugenzi Mtendaji wa AUWSA, Mhandisi Justine Rujomba amesema katika Jiji la Arusha hali ya upatikanaji wa maji ni asilimia 99, kwa saa 21 kwa siku na lengo ni kuhakikisha upatikanaji wake unakuwa kwa saa 24.
Rujomba amesema mabadiliko ya tabianchi yanasababisha ukosefu wa maji, akisema chemchem nyingi zimepunguza uzalishaji wa maji, suala ambalo limeifanya Serikali kuanza kuchimba visima ili kusaidia kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi.
“Moja ya changamoto kubwa ni za wizi wa maji na wanaoiba ni wale wenye pesa, uchakavu wa baadhi ya miundombinu unaosababisha upotevu wa maji,” amesema.
Kaimu Meneja wa Ruwasa Mkoa wa Arusha, Mhandisi Magai Kakuru amesema upatikanaji wa maji katika halmashauri sita za Mkoa wa Arusha ni asilimia 74.3 na wilaya ambazo zimeathirika na mabadiliko ya tabianchi na kusababisha upungufu wa maji ni Monduli, ambako miradi mbalimbali inatekelezwa kupunguza tatizo hilo.