KIPA wa Singida Black Stars, Metacha Mnata amesema msimu huu anaitaka ile tuzo ya kipa bora wa Ligi Kuu Bara iliyochukuliwa na Ley Matampi wa Coastal Union msimu uliopita.
Metacha ameliambia Mwanaspoti kwamba, msimu huu anataka kuwa na clean sheet nyingi zitakazomfanya aibuke kinara miongoni mwa wa makipa wa ligi hiyo.
“Msimu huu natamani kuandika rekodi za clean sheet nyingi kama ilivyokuwa kwa makipa wengine ambao walifanya vizuri kama Ley Matampi wa Coastal Union na Djigui Diarra wa Yanga (msimu uliopita). Ili nifanikishe hilo inaanzia ushindani ndani ya kikosi,” alisema kipa huyo wa zamani wa Yanga.
Metacha alisema kitendo cha Matampi kuongoza kwa kuwa na clean sheet 15 msimu uliopita baada ya kucheza mechi 24 za ligi kimetoa somo kwamba hakuna linaloshindikana mbele ya safari kwa kujituma.
“Napenda ushindani unaomfanya mchezaji asijibweteke. Ukiondoa Simba, Yanga na Azam FC, Singida Black Stars ina wachezaji wenye uwezo mkubwa utakaotufanya tuwe washindani dhidi ya wapinzani wetu,” alisema.
Kipa huyo alisema kikosi cha Singida Big Stars kinampa matumani makubwa ya kufanya vizuri kwenye ligi kutokana na wachezaji waliosajiliwa na anaamini kila nafasi ina ushindani ambao kwake anauchukulia kama chachu ya kuongeza bidii.
Metacha aliyejiunga na timu hiyo akitokea Yanga, alisema Singida ina wachezaji wenye uwezo mkubwa ambao wanaweza kuifanya imalize katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa mashindano hayo msimu huu.