Ngushi afungua kitabu cha mabao Ligi Kuu Bara

MSHAMBULIAJI wa Mashujaa FC ya Kigoma, Crispin Ngushi amekuwa mchezaji wa kwanza kwa msimu huu kufunga bao katika mechi za Ligi Kuu Bara 2024-2025 wakati akiitanguliza Mashujaa kwenda mapumziko ikliwa mbele kwa bao 1-0 dhidi ya Dodoma Jiji.

Ngushi ambaye amewahi kutamba na timu za Mbeya Kwanza aliyopanda nao Ligi Kuu misimu mitatu iliyopita, kabla ya kutua Yanga na baadae kuichezea Coastal Union msimu uliopita amefunga bao hilo dakika ya 33 ya pambano hilo linalopigwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, mjini Kigoma.

Bao hilo limemfanya nyota huyo kuingia katika orodha ya kuwa mchezaji wa kwanza msimu huu kufunga bao baada ya jana timu za Pamba Jiji na Tanzania Prisons kufungua msimu na kushindwa kufungana.

Pamba na Prisons zilivaana jana kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza ikiwa ni mchezo pekee uliopigwa katika ufunguzi wa msimu na kufanya iwe ni mara ya kwanza kwa misimu ya karibuni kutumika zaidi ya dakika 90 kabla ya kufungwa bao la kwanza la msimu.

Msimu uliopita, Elias Maguri ndiye aliyefungua pazia ya mabao akiwa na Geita Gold alipofunga bao pekee wakati timu hiyo iliyoshuka daraja kwa sasa kuizamisha Ihefu ikiwa ugenini jijini Mbeya na nyota huyo hakufunga tena hadi msimu ulipoisha na timu na Mtibwa Sugar zikienda Ligi ya Championship.

Huu ni msimu wa pili kwa Mashujaa kucheza Ligi Kuu Bara baada ya kupanda daraja msimu uliopita na kumaliza ikiwa nafasi ya nane.