LONDON, ENGLAND: LISEMWALO ni kwamba kuna uwezekano mkubwa kutokea dili kubwa la kubadilishana wachezaji, litakalomshuhudia straika Romelu Lukaku akienda Napoli na mwenzake, Victor Osimhen akitua Chelsea.
Bila shaka ni dili linalosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka wa huko Ulaya. Kinachoelezwa ni kwamba, Chelsea inahitaji huduma ya straika mpya kwenye kikosi chao na wanamtazama Osimhen mwenye thamani ya Pauni 85 milioni kama mchezaji atakayefaa.
Lakini, huko Napoli anakocheza Osimhen ametua kocha mpya, Antonio Conte, ambaye hajaweka kizuizi cha mshambuliaji huyo kuondoka, lakini anachohitaji aletwe straika Lukaku, ambaye alimsajili wakati alipokuwa akifanya kazi Stamford Bridge.
Itakuwaje? Dili hilo la Lukaku na Osimhen siyo lenyewe tu linalodaiwa linaweza kutokea dirisha hili kwa maana ya wachezaji hao kupishana. Kinachosemwa staa wa Atletico Madrid, Joao Felix anaweza kuhusika pia kwenye dili la kubadiliana na Conor Gallagher wa Chelsea.
Kwenye dirisha hilo, Chelsea imeonekana kuwa na mpango wa kufanya dili za kubadiliana wachezaji baada ya kuripotiwa pia inamtaka Jadon Sancho wa Manchester United kwa kubadilishana na wachezaji wawili pamoja na pesa juu. Dirisha la usajili wa majira ya kiangazi kwa England litafungwa Agosti 30 na bila shaka itakuwa sehemu nyingi za Ulaya.
Kilichopo kwa mashabiki ni kusubiri kuona kama kitatokea kitu kwenye dili hizo za kubadilishana wachezaji.
Katika mchezo wa soka zimeshawahi kutokea dili 11 matata za kubadilishana wachezaji ambazo zimekuwa maarufu hadi zama hizi. Hivyo, hakuna kinachoshindikana juu ya uwezekano wa kutokea dili za aina hiyo.
11. Francesco Coco & Clarence Seedorf
Ni dhambi kutaja jina la Seedorf bila ya kuonyesha makali yake aliponyakua makombe ya Ulaya mara nne akiwa na klabu tatu tofauti. Kiungo huyo wa Kidachi mataji yake mawili kati ya hayo alibeba alipokuwa na kikosi cha Inter Milan. Mwaka 2002, Inter iliamua kumuuza mchezaji huyo katika dili lililomhusisha pia kubadilishana na mchezaji, wingback wa kushoto, Francesco Coco. Hivyo, Seedorf alikwenda AC Milan na Coco alitua Inter. Huko AC Milan, alikwenda kushinda taji jingine la Ligi ya Mabingwa Ulaya, huku Coco akiwa mzigo tu huko Inter.
10. Diego Simeone & Christian Vieri
Kwenye Serie A dili za kubadilishana wachezaji kimekuwa kitu cha kawaida. Klabu zake zinapenda sana kufanya dili za kubadilishana na na moja ya dili za kibabe iliwahusisha mastaa Diego Simeone na Christian Vieri ambapo walipishana kwenye klabu za Lazio na Inter Milan katika dirisha la majira ya kiangazi 1999. Inter iliongeza pesa, ilipolipa Pauni 28 milioni na kufanya thamani ya Vieri kipindi hicho kufikia Pauni 57 milioni. Vieri alifanya vizuri Inter alipofunga mabao 103 katika mechi 143. Simeone aliisaidia Lazio kushinda Scudetto msimu wa 1999-00.
9. Diego Milito, Thiago Motta, Leonardo Bonucci na wengine wanne
Bila shaka kuna mtu anafahamu kilichotokea wakati Samuel Eto’o alipohama kutoka Barcelona kwenda kuunda kikosi matata kabisa cha Inter Milan chini ya Mreno Jose Mourinho na kufanikiwa kubeba mataji matatu makubwa ndani ya msimu mmoja, 2009-10. Inter Milan wakati huo ilikuwa pia na mastaa Diego Milito na Thiago Motta kutoka Genoa. Kipindi hicho, kinda Leonardo Bonucci alitoka Inter kwenda upande wa pili, sambamba na Robert Acquafresca, Francesco Bolzoni na Riccardo Meggiorini huku straika Ivan Fatic naye alihusika.
8. Julio Baptista & Jose Antonio Reyes
Hayati Jose Antonio Reyes, fundi wa mpira wa Kihispaniola alirejea kwao Hispania baada ya misimu kadhaa ya kukumbukwa kwenye kikosi cha Arsenal mwaka 2006. Hilo lilikuwa dili la kubadilishana kwa mkopo. Reyes alitumikia msimu mmoja Real Madrid, ambapo alifunga mabao saba na kuasisti mara nne huku akishinda taji la La Liga. Huko Arsenal, ambako alipishana na Julio Baptista, Mbrazili huyo alifunga mabao 10, manne yalikuwa kwenye mechi moja ya Liverpool na aliasisti pia mara nne, lakini alishindwa kuipa The Gunners taji lolote. Dili lilikufa msimu ulipoisha.
7. Ashley Cole & William Gallas
Utacheka, lakini huo ndio ukweli, Ashley Cole alishinda mataji mengi ya Ligi Kuu England akiwa Arsenal kuliko alipokuwa na Chelsea. Beki huyo wa kushoto, alishinda taji moja tu la Ligi Kuu England kwa kipindi chake cha miaka minane aliyocheza huko Stamford Bridge. Lakini, dili lake la kutoka Arsenal lilimhusisha beki mwingine, William Gallas, ambaye alienda upande wa pili. Cole alishinda pia Ligi ya Mabingwa Ulaya, Europa League, Kombe la Ligi na mataji kadhaa ya Kombe la FA akiwa na Chelsea, wakati Gallas hakuna cha maana alichofanya Arsenal.
6. Ricardo Quaresma & Deco De Souza
Baada ya kushindwa kufanya vizuri Barcelona ambako mabosi waliamini kwa kumsajili yeye na kuachana na Cristiano Ronaldo, Ricardo Quaresma alirudi Ureno kwenda kujiunga na mabingwa wa Ulaya kwa kipindi hicho, FC Porto. Kipindi hicho, Deco, alikuwa staa wa Porto, hivyo dili la Quaresma kurudi Ureno lilimfanya kiungo Deco atue zake Nou Camp, ambako alikwenda kuwa mchezaji muhimu alipoipa La Blaugrana ubingwa wa La Liga kwa misimu miwili mfululizo la Ligi ya Mabingwa Ulaya 2006. Lakini, Porto ililipwa pia Pauni 13 milioni ukimweka kando Quaresma.
5. Alexis Sanchez & Henrikh Mkhitaryan
Unakumbuka ile video ya utambulisho wake akionekana akipiga piano na kuonekana kama Alexis Sanchez angekwenda kuwa mchezaji hatari zaidi Manchester United alipohama kutoka Arsenal. Dili hilo lilimshuhudia kiungo wa Man United, Henrikh Mkhitaryan akienda upande wa pili na hakika alikwenda kuwa na mchango mkubwa huko Emirates kuliko Sanchez huko Old Trafford. Dili hilo lilidaiwa kuwa na thamani ya Pauni 35 milioni, kwamba Man United ilimchukua Sanchez na Arsenal ilimbeba Mkhitaryan kwa maana thamani zao zilikuwa sawa.
4. Luis Garcia & Fernando Torres
Staa Luis Garcia aliondona Liverpool kwenda Atletico Madrid katika dili lililomhusisha Fernando Torres kutua Anfield. Kilichoelezwa ni kwamba Liverpool ililipa pia Pauni 21.5 milioni pamoja na Garcia ili kumpata straika Torres. Baada ya kutua Anfield, Torres alikuwa moto kwelikweli na kuwa kipenzi cha mashabiki, lakini kwa bahati mbaya hakufanikiwa kushinda taji lolote, huku mabao yake yaliifanya Liverpool ya kipindi hicho chini ya kocha Rafael Benitez kushindania ubingwa kwenye msimo wa 2008-09.
3. David Luiz & Nemanja Matic
Ilivutia kuona wawili hao wakicheza pamoja huko Stamford Bridge, katika awamu yao ya pili kwenye kikosi cha Chelsea, lakini kabla ya hapo, wakali hao walipishana, mmoja akitokea Benfica kwenda Chelsea na mwingine kinyume chake. Chelsea ilimchukua Luiz kutoka Benfica mwaka 2011 katika dili lililomhusisha Matic. Luiz aliisaidia Chelsea kushinda taji la Ligi ya Mabingwa kwenye msimu wake wa kwanza, kisha aliongeza mataji mengine kama Europa League, Kombe la FA na Ligi Kuu England. Matic baada ya kung’ara Estadio da Luz, alirejea Chelsea mwaka 2014.
2. Miralem Pjanic & Arthur
Hii imekuwa kubwa zaidi kutokana na ada ya uhamisho iliyolipwa. Arthur anatazamwa kama mchezaji aliyeuzwa ghali zaidi na klabu ya Barcelona, wakati aliponaswa na Juventus kwa ada ya Euro 80 milioni, huku kiungo Miralem Pjanic naye akiingia kwenye 10 bora ya usajili wa pesa nyingi, Euro 60 milioni. Pjanic kwa sasa ni mchezaji huru baada ya mkataba wake wa miaka miwili huko Falme za Kiarabu katika klabu ya Sharjah. Arthur bado yupo Juventus, lakini haonekani kuwa kwenye mipango yao baada ya kumtoa kwa mkopo Liverpool na Fiorentina.
1. Zlatan Ibrahimovic & Samuel Eto’o
Kilikuwa kitu cha kuvutia kuona wachezaji wawili waliokuwa kwenye viwango bora kabisa wakipishana kwenye dili la kubadilishana wachezaji mmoja akienda Barcelona na mwingine akinaswa Inter Milan. Eto’o alitoka Barcelona kwenda Inter na Zlatan ilikuwa kinyume chake. Eto’o alikwenda kushinda mataji matatu makubwa ndani ya msimu kwa msimu wa pili mfululizo baada ya kutoa Inter, wakati Ibrahimovic alishinda ubingwa wa La Liga huko Barcelona na kufunga mabao 22 katika mechi 46 kabla ya kutibuana na kocha Pep Guardiola na kujiunga AC Milan.