Tanzania Prisons yageukia straika haraka

ACHANA na matokeo ya pointi moja waliyovuna ugenini dhidi ya Pamba Jiji, benchi la Tanzania Prisons limesema linahitaji kuongeza makali eneo la ushambuliaji kabla ya higi haijachanganya.

Prisons ilianzia ugenini kukipiga na Pamba Jiji katika mchezo wa Ligi Kuu, ambapo mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza, iliisha kwa suluhu ya bila kufungana.

Kocha msaidizi wa timu hiyo, Renatus Shija alisema pamoja na kuambulia pointi moja, haikuwa malengo yao kutokana na namna walivyokuwa wameandaa kikosi chao.

Alisema kwa jicho la benchi la ufundi, waliona kasi kuwa ndogo kwenye eneo la ushambuliaji kwa kushindwa kutumia vyema nafasi walizopata akieleza kuwa wanaenda kuongeza mbinu ili mechi ijayo dhidi ya Mashujaa wafanye kweli.

“Tuliwaheshimu wapinzani lakini tulishindwa kutumia vyema nafasi tulizopata, benchi tumeona wapi turekebishe ili mchezo ujao tupate ushindi wenye idadi kubwa ya mabao,” alisema Shija.

Alisema pamoja na udhaifu huo, vijana walionyesha uwezo na kuipambania timu akieleza kuwa kabla ya mchezo wao ujao dhidi ya Mashujaa, Agosti 23 huko mkoani Kigoma, watajisahihisha ili kufikia malengo.

Kipa wa timu hiyo, Mussa Mbisa alisema pamoja na matokeo hayo, bado mwanzo si mbaya kwakuwa kila timu Ligi Kuu imejipanga na kwamba kwa sasa wanaelekeza nguvu kwenye mechi ijayo.

“Pointi moja ya ugenini siyo mbaya, japokuwa tulipambana kusaka ushindi ila haikuwa bahati kwetu, timu zote zimejipanga na tunaelekeza nguvu mchezo ujao,” alisema nyota huyo.