MARACANAZO: Simulizi nzito ya ubabe wa Uruguay kwa Brazil

MFANYABIASHARA wa mji wa Rio de Janeiro, Brazil alitakiwa na serikali kutafuta jina jipya la duka lake na kuondoa lile la ‘Februari 24’ ili kunusuru maisha yake.

Hii ni kwa sababu Februari 11, mwaka huu Argentina waliwafunga Brazil na kuwanyima fursa ya kucheza fainali za kandanda za Olimpiki zilizofannyika Paris, Ufaransa. Brazil iliyotarajia kutetea ubingwa wa kandanda wa Olimpiki baada ya kubeba kombe 2016 na kulitetea 2020, iliondolewa na mahasimu wake Argentina kwa kufungwa bao 1-0. Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa nchi hiyo kutoshiriki fainali hizo tangu 2004.

Kabla ya hapo Argentina iliifunga Brazil bao 1-0 katika robo fainali ya Kombe la Copa America. Matokeo hayo  yalisababisha watu wa Brazil kuuona mwaka 2024 ni kama wa maafa kwa sababu wanapenda kandanda kuliko kitu kingine chochote.

Wakati bendera za nchi nyingi zimewekwa jua, nyota au mwezi, ile ya Brazil ndiyo nchi pekee duniani ambayo bendera yake ina mpira katikati.

Hivi sasa watu wa Brazil wanaumia na kile wanachokieleza kama maafa ya kitaifa kwa vile hata timu ya kandanda ya wanawake licha ya kumiliki mchezo ilifungwa na Marekani katika fainali za Olimpiki.

Kuanzia miaka ya 1960 hadi 1990 Brazil ilikuwa kileleni katika viwango vya Shirikisho la Kandanda la Kimataifa (Fifa) na mara chache ilishika nafasi ya pili au ya tatu, lakini sasa ipo ya tano. Argentina inaongoza na kufuatiwa na Ufaransa, Hispania na England.

Brazil imepata maafa ya kila aina yakiwemo mamia ya watu kupoteza maisha kutokana na mafuriko na milipuko ya magonjwa mbalimbali katika miaka 100 iliyopita, lakini kwa watu wake maafa yasiyosahaulika ni ya kufungwa katika michezo muhimu ya kandanda.

Miongoni mwa yanayohesabika kama maafa makubwa ni ya tukio lijulikanalo kama Maracanazo (kipigo katika uwanja wao wa mpira wa Maracana) mwaka 1950. Maafa hayo ni ya kufungwa mabao 2-1 katika fainali ya Kombe la Dunia mwaka 1950.

Kitendo cha yule mfanyabiashara kulipa duka lake jina la Februari 24 kilizua hasira nchi nzima na baadhi ya watu katika mitandao ya kijamii waliahidi kumuua kwa kufanya utani wakati nchi ikiwa katika msiba wa kufungwa na Argentina na baadaye kinamama kupoteza kombe dhidi ya Marekani.

Katika fainali za Kombe la Dunia za 1950, Brazil iliyokuwa mwenyeji ilipocheza na Uruguay ilikuwa ya kwanza kupata bao lililofungwa na Albino Cardoso katika dakika ya 47.

Wakati Brazil ilihitaji sare tu ili ibebe kombe, Uruguay ilisawazisha katika dakika ya 66 kupitia winga machachari Juan Schiaffino na Brazil ilijibu mashambulizi, lakini ikajikuta inapachikwa bao la pili lililoipatia ushindi Uruguay katika dakika 79 na kubeba kombe.

Bao lile lilielezwa na watu wa Brazil kuwa sawa na bomu la nyuklia lililoripuliwa Hiroshima, Japan, wakati wa Vita Kuu vya Pili vya Dunia 1945 na kuua maelfu ya watu.

Mfungaji wa bao lililoinyima Brazil kombe ni Alcides Ghiggia aliyekuja kujulikana mpaka kufa kwake Julai 16, 2015 akiwa na miaka 89 kwa jina la Maracanazo (kipigo cha uwanja wa Maracana).

Bomu la Hiroshima lilitupwa Hiroshima na Marekani Agosti 6, 1945 mwishoni mwa Vita Kuu vya Pili vya Dunia na kuua watu 130,000. Siku hizi kila Brazil ikifungwa katika kandanda watu wa nchi hiyo husema Maracanazo amefufuka na kuleta maafa mengine.

Kilichotokea katika Uwanja wa Maracana kimeandikiwa vitabu, kutungiwa mashairi na kutengezewa filamu ya sinema iitwayo Maracanazo. Filamu fupi ya mchezo unaoitwa Maracanazo inaonyeshwa kwa watu wa Brazil kandanda ni sawa na ibada.

Filamu hiyo inaonyesha watu wengi walijiua kwa kuona aibu na wengine walikufa kwa mshituko wa moyo ilhali wengine walikuwa na maombolezo ya miezi na timu ya Brazil ilikaa miaka miwili bila ya kucheza hata mchezo mmoja kuomboleza kipigo cha Maracana.

Wachezaji wengi wa kikosi kilichochapwa katika Uwanja wa Maracana waliamua kuacha kuchezea timu ya taifa kwa kuhofia kuhatarisha maisha wakitaja kufungwa na Argentina au Uruguay. Katika filamu hiyo mfalme wa kandanda duniani, Edson Arantes do Nascimento (Pele), anasema siku ile akiwa na miaka 10 ilikuwa ni mara ya kwanza kumuona baba yake analia kama mtoto mdogo, sawa na yeye alipochapwa na baba.

Pele anasema kila alipokwenda alikuta watu wamejawa huzuni na kwa wiki nzima walikatazwa kucheza kandanda mitaani kwa vile taifa lilikuwa katika maombolezo.

Huu ndio ule tunaoweza kuuelezea kama wazimu wa mchezo wa kandanda katika baadhi ya nchi duniani na hasa Brazil, ambapo watu wengine anapozaliwa mtoto wa kiume zawadi wanayopeleka ni chandimu.

Hali hiyo ndiyo iliyosababisha kutoshangaa kuona bendera ya Brazil ina mpira katikati kuonyesha ushabiki na mapenzi yaliyovuka mpaka ya watu wa nchi hiyo kwa kandanda.

Kama yupo mtu aliyesikitikia zaidi maafa ya Maracana ni huyo aliyepewa jina la Maracanazo (Albino Friaça Cardoso) na mara nyingi baada ya kutoa kile kipigo aliomba kuutembelea Brazil kuwaomba radhi watu wa nchi hiyo kwa maafa aliyosababisha katika mchezo wa fainali.

Nyota huyo alikataliwa kwa sababu ingekuwa kama kuchoma msumari wa moto juu ya kidonda na zaidi kwa sababu maisha yake yangekuwa hatarini. Hatimaye kama kuonyesha  imesahau machungu Brazil ilimualika mwanzoni mwa mwaka 2000 na kumpa heshima ya kuonyesha kiichotokea Maracana kuwa ni sehemu ya mchezo wa kandanda.

Ghiggia alikwenda katika Uwanja wa Maracana na kuzindua kumbukumbu ya sanamu lake lililojengwa hapo pamoja na sanamu za wachezaji watatu mashuhuri duniani. Hawa ni Pele, Franz Beckenbeur wa Uholanzi na Eusebio da Silva Ferreira wa Ureno (mzaliwa wa Msumbiji). Alipozindua sanamu hizo alitokwa na machozi na kusema: “Nawaomba msamaha wananchi wa Brazil.”

Ghiggia alikuwa akisema anaikumbuka siku ile kwa mchanganyiko wa furaha na majonzi. Furaha ilitokana na kuisaidia Uruguay kubeba kombe na huzuni kutokana na maafa aliyosababisha. Siku ile aliyozidua Ghiggia aliyekuwa  anacheza winga ya kulia alikwenda sehemu aliyoupokea mpira na kufyatua mkwaju ambao kipa Moacir Bardosa alishindwa kuuzuia.

Aliuweka mpira chini, akaubusu na kutamka: “Nawaomba samahani wananchi wa Brazil” na mpaka alipokaribia kuaiga dunia kipa Bardosa hakuwa na furaha kwani kila alipokwenda alizomewa kama mhalifu. Siku chache kabla ya kifo chake  mwaka 2000 aliwaambia watu wa Brazil kwamba hatawasamehe kwa waliyomfanyia hata akiwa kaburini.

“Inasikitisha kuona hata watoto waliozaliwa miaka 30 baada ya maafa ya Maracana wananizomea kama vile nilikuwa jambazi lilioua watu. Laiti ningelijua nisingekubali kuichezea timu ya Brazil,” aliliambia gazeti moja la Brazil.

Alisema adhabu kali ya uhalifu Uruguay ilikuwa kifungo jela cha miaka 30, lakini aliadhibiwa kwa zaidi ya miaka 50. Uruguay ilipozu kucheza fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika Brazil 2014, wachezaji walikwenda kumuomba Ghiggia kuipa baraka za kwenda kucheza Uwanja wa Maracana.

Ghiggia alikataa na kusema hakutaka kurejesha wimbi jipya la machungu kwa watu wa Brazil na zaidi kwa vile  alishachukua uraia wa Italia. Alipoulizwa alitarajia timu gani ingelibeba Kombe la Dunia katika mashindano alisema Ujerumani kwa sababu ilikuwa na wachezaji wazuri, hasa wale waliotoka Bayern Munich.

Utabiri wake ulikuwa sahihi na Ujerumani ilibeba kombe kwa kuifunga Argentina bao 1-0 katika fainali baada ya kuichapa Brazil 7-1 katika nusu fainali. Fifa ilimualika Ghiggia kwenda Brazil na muda mwingi aliangalia michezo iliyofanyika katika Uwanja wa Maracana na alizuru kaburi la kipa Bardosa na kuonana na watoto wake.

Alcides Edgardo Ghiggia ambaye alizaliwa Desemba 22, 1926 katika mji wa Montevideo, Uruguay alikuwa mmoja wa mawinga wa kulia machachari katika miaka ya 1950 na alichezea timu za Uruguay 1950-1965 na Italia 1957-1959.

Aliwahi kuichezea timu ya CA Penarol ya Uruguay 1948 akiwa na miaka 21 na 1952 alifungiwa kwa mwaka mmoja kwa kumtwanga makonde mwamuzi aliyekataa bao alilofunga. Aliporudi uwanjani 1953 aliichezea AS Roma katika Ligi Kuu Italia (Serie A) na kuwa nahodha katika msimu wa 1957/58, na baadaye aliichezea AC Milan na kustaafu akiwa na Danubio ya Uruguay aliyoichezea kuanzia 1962 hadi 1968. Kwa muda mfupi mwaka 1980 alikuwa kocha wa CA Peñarol.

Akisherehekea miaka 80 tangu kuzaliwa, Ghiggia alipewa heshima na Bunge la Uruguay na nchi hiyo ilitoa stempu yenye picha yake na kutungiwa wimbo ambao unapendwa Uruguay unaoitwa Maracanazo. Mnamo Juni 15, 2012 alipata ajali na kuwa mahatuti kwa wiki nzima baada ya gari lake kugongana uso kwa uso na lori la mizigo nje kidogo ya Jiji la Montevideo.

Mkongwe huyo alivunjika mguu na kupata maumivu ya mgongo na kifua, na alipotoka hospitali baada ya miezi mitatu alisema kwake ile ajali ndio “Maracanazo”.