INAWEZA kuonekana kuwa Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) halitaki masuala yake yapelekwe mahakama za kiraia kwa ajili ya kufanyiwa uamuzi, lakini si kila jambo haliendi mahakamani.
Kuna masuala ambayo Fifa yenyewe inajiona haina mamlaka ya kuyashughulikia, hivyo kuyaacha yafanywe na vyombo vya kiserikali. Masuala kama ya kughushi, haki ya kufanya kazi kama ile iliyomsukuma Marc Bosman kupinga kanuni za mpira wa miguu zilizokuwa zinazuia mchezaji aliyemaliza mkataba wake kuondoka klabuni bila ya ada yoyote.
Yapo masuala kama ya rushwa ambayo ni vigumu kwa Shirkisho la Soka Tanzania (TFF) pekee kufanyia uchunguzi na kuthibitisha kuwa kulikuwa na rushwa hadi chombo maalumu kwa ajili ya kazi hiyo kibebe jukumu. Hata yule refa wa Ujerumani, Robert Hoyzer alishughulikiwa katika mahakama ya kawaida na kubaini mwamuzi huyo alihusika katika kashfa ya kupanga matokeo iliyohusisha Euro 2 milioni.
Hivi ndivyo suala la kiongozi wa zamani wa Chama cha Soka cha Tabora, Yusuf Kitumbo alivyoingia kwenye kashfa ya kupanga matokeo ya mechi za ligi daraja la kwanza, wakati huo, kwa nia ya kutaka kuiwezesha timu yake ipande daraja.
Baadhi ya wachezaji walikiri kuwa walitumiwa fedha na kiongozi huyo kwa njia ya simu kwa ajili ya kupanga matokeo. Lakini suala hilo lilichukuliwa na Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa (Takukuru) na Kitumbo alifunguliwa kesi mjini Gairo.
Lakini ninavyofahamu, kesi hiyo ilishaisha tangu mwaka jana na si Takukuru, wala kampuni ya simu ambayo ilidaiwa fedha hizo zilipitishwa, na wala si wachezaji walioweza kuthibitisha kuwa kulikuwepo na mpango huo wala ushahidi wa kielektroniki kuwa kuna fedha zilitumwa.
Kwa mujibu wa nyaraka za kesi hiyo, hakimu hakufurahishwa na jinsi maofisa wa Takukuru walivyoshughulikia suala hilo na kwenda mahakamani bila ushahidi, kitu alichokiona kama ilikuwa ni njama za kumuonea mtuhumiwa.
Kwa maana nyingine, Kitumbo hakutiwa hatiani na chombo hicho mahsusi kwa ajili ya kuzuia na kupambana na rushwa na ambacho kimejaliwa maofisa wenye stadi na elimu ya kushughulikia tatizo hilo baya kwenye jamii.
Ajabu ni kwamba hadi sasa TFF haijaondoa adhabu iliyompa Kitumbo ya kufungiwa maisha kujihusisha na soka pamoja na wahusika kutoweza kuthibitisha mahakamani kwamba Kitumbo alihusika kuhonga wachezaji kwa manufaa ya klabu yake.
Kibaya zaidi ni kwamba wakati kesi imeisha bila ya kiongozi huyo kutiwa hatiani, TFF inatoa taarifa ya kuzuia viongozi wa Tabora United kushirikiana na Kitumbo katika uendeshaji wa timu hiyo.
Nadhani kama TFF ina ushahidi zaidi ya uliotakiwa mahakamani, ingeomba kuwa sehemu ya mashahidi katika kesi hiyo ili ithibitishe kuwa kulikuwa na mpango rasmi wa kupanga matokeo, lakini kama iliachia chombo pekee nchini kinachotambulika kisheria kuchunguza masuala ya rushwa na shauri lake likapelekwa kwenye chombo cha haki, basi Kitumbo hastahili tena kuendelea kutumikia adhabu iliyotolewa kwa fikra au tuhuma tu za kupanga matokeo.
Najua TFF inaelekea kwenye uchaguzi na hivyo huu ni wakati wa kupanga rasmi safu zake za wapiga kura na kuwaweka mbali watu wenye ushawishi mkubwa. Si vibaya kujipanga kwa uchaguzi kwa njia zilizo halali, lakini kutumia mamlaka kuwaweka mbali watu wanaoonekana tishio, si kitu kizuri.
Sioni kitu tofauti ambacho Kitumbo anaweza kuwa anaadhibiwa zaidi ya siasa za uchaguzi na hii imetokea mara kadhaa kwa kiongozi huyo kujikuta kwenye matatizo kama hayo. Naona wazi kuwa yale mambo ya kupelekana mahakamani kwa sababu ambazo ni za kimpira badala ya zile nilizozitaja hapo juu, yameanza kurejea taratibu.
Mbali na hayo, kuna mwamuzi alienda mahakamani kudai haki zake, kuna kijana ambaye amefungua kesi kupinga uhalali wa kanuni zinazotumika sasa kuadhibu watu na si ajabu kama Kitumbo ataenda mahakamani kupinga adhabu aliyopewa kinyume cha sheria za nchi ambazo zinataka mahakama pekee ndiyo ithibitishe jinai yoyote.
Kama kweli kuna tatizo, basi TFF ingefungua shauri jingine dhidi ya Kitumbo na kumshtaki kwenye vyombo vyake vya haki ili vitoe uamuzi mwingine tofauti na ule uliopigwa chini na mahakama.
Na hii itawezekana tu pale vyombo vya haki vitakapokuwa vinatoa adhabu pale inapothibitika bila ya shaka yoyote kuwa mtuhumiwa alihusika. Kama uthibitisho huo unatakiwa uchakatwe na chombo cha haki cha kiraia, basi ni lazima familia ya mpira iheshimu uamuzi huo na kuyatekeleza kadiri yalivyoamuliwa.
Lakini kuendeleza adhabu ambayo kosa lake halikuthibitika mahakamani, ni kupuuza utawala wa sharia na kupuuza uamuzi wa vyombo vya haki. Na tukijenga utamaduni huo, nani ataamini kwamba vyombo vyetu vya haki katika mpira wa miguu vinatenda haki?
Ni lazima Haji Manara ataeleweka pale atakapopiga kelele kuwa hakutendewa haki, hali kadhalika kijana anayeitwa Katabazi atalalamika, na wengine. Ambao hawatalalamika ni wale waliopewa adhabu wasijihusishe na mpira wa miguu, lakini wanaendelea kujihusisha halafu maofisa wa TFF wanawachekea au wale walioadhibiwa halafu baada ya mwezi mmoja wakapunguziwa adhabu kwa kiwango kikubwa.
Siku zote ni muhimu haki itawale na watu waamini katika vyombo vya haki vya mpira wa miguu badala ya kuvichukulia kama fimbo ya viongozi kutandika watu wanaonekana kuwa tishio katika harakati zao za kutaka madaraka hata kama watu hao hawagombei uongozi.
Kama tuliamua kuondoa masuala ya mpira wa miguu mahakamani kwa kuwa tuna vyombo vya haki, basi haki itendeke bila ya aina yoyote ya upendeleo, ubaguzi au hila za kumfunga mtu mikono apungukiwe nguvu za kupambana.