Ngumi za kulipwa zapelekwa Songea

TAMASHA kubwa la ngumi za kulipwa mkoa wa Ruvuma limepangwa kufanyika Septemba 8 kwenye Uwanja wa Majimaji, mjini Songea.

Muandaaji wa tamasha hilo, Jofrey Miti  ya Lizaboni alisema kuwa mapambano mbalimbali ya ngumi za kulipwa yatafanyika katika tamasha hilo lililopangwa kuanza saa 11.00 jioni na litasindikizwa na mapambanio kadhaa likiwamo la bondia Chidi Benga wa Songea dhidi yaMbwana ‘Van Damme’ Ally wa Dar es Salaam katika uzito wa Super Middle.

Alisema pambano jingine ni lile la James Ntanga wa Songea dhidi ya James Kiyeyeu wa Iringa katika pambano la raundi sita la uzito wa Super Light, huku kwenye uzito wa cruiser, Doza Mnyama wa Songea atazipiga na Sadi Tompoo wa Dar es Salaam.

Bondia Taimu Saidi akipanda ulingoni kupambana na  Alex “Big Dad” Phillemon wa Mbeya katika pambano la raundi sita la uzito wa juu, Heavyweight, huku uzito wa super light la mabondia wa kike kati ya Fatuma Yazidu wa Dar es Salaam dhidi ya Suzana Mhagama wa Iringa  na bondia Mussa Chitepete wa Songea atapambana na Festo Chipona wa Dar es Salaam.

Kwa upande mratibu wa  tamasha hilo, bondia wa zamani, Omari Yazidu alisema maandalizi yote muhimu yanaendelea vizuri na kuwataka wadau wa mchezo wa ngumi za kulipwa kufika kwa wingi siku ya tamasha hilo.

“Tunatarajia kuwa na mapambano makali yenye ushindani wa hali ya juu. Tunatarajia Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini, Damas Ndumbaro ambaye ni Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, wakuu wa wilaya zote za mkoa wa Ruvuma pamoja na Wabunge wote wa majimbo ya uchaguzi kuhudhuria tamasha hilo,” alisema Yazidu.