WAGANDA wataendelea kumuota Mtanzania Madina Idd katika viwanja vyao vya gofu vilivyopo katika miji ya Kampala na Entebbe baada ya Mtanzania huyu shupavu kuviteka vyote katika kipindi cha siku saba tu.
Madina ameibuka mshindi wa jumla wa michuano ya wazi ya wanawake nchini Uganda yajulikannayo kama John Walker akimshinda Mtanzania mwenzake Hawa Wanyeche kwa mikwaju miwili katika mashindano yaliyochezwa katka mashimo 54 ya viwanja vya gofu vya Entebbe kuanzia Alhamisi, Agosti 22 hadi Jumamosi, Agosti 24 mwaka huu.
“Yalikuwa mashindano magumu na yenye upinzani mkali kwani Waganda, akiwemo bingwa mtetezi Martha Babirye, walipania kufanya vizuri ili kujenga heshima katika viwanja vyao. Nashukuru mambo yalikuwa mazuri katika siku ya pili na ya tatu ya mchezo ambapo niliweza kuleta matokeo bora,” alisema Madina ambaye ni mwanachama wa klabu ya Gymkhana ya Arusha.
Siku saba nyuma, Madina alishinda mashndano mengine ya wazi yaliyofanyika mjini Kampala baada ya kumshinda Mganda Peace Kabasweka kwa mikwaju mitano.
Madina alyeanza mashindano kwa kushika nafasi ya nne nyuma ya Mtanzania Hawa Wanyeche aliyeongoza kwa mikwajui 74 na kufuatiwa na Mganda Martha Babirye aliyerudisha mikwaju 75 na Neema Olomi alyepiga mikwaju 76, alicharuka siku ya pili ya pili na ya tatu na kuwashinda wote kwa jumla ya mikwaju 228 aliyoipiga katika siku tatu za michuano hiyo.
Alipiga mikwaju 78 siku ya kwanza na kujiimarisha kwa mikwaju 76 siku ya pili kabla ya kuwafunika wote kwa mikwaju 74 katika mashimo 18 ya mwisho siku ya Jumamosi.
Mganda Martha Babirye ambaye alikuwa ndiye bingwa mtetezi, hakuweza kufua dafu kwa Watanzania baada ya kumaliza wa tatu nyuma ya Mtanzania Wanyeche aliyemaliza wa pili baada ya kuongoza kwa mkwaju mmoja siku ya kwanza ya mashindano.
Wanyeche alimaliza na jumla ya mikwaju 230 wakati Babirye aliweza kutengeneza mikwaju 232.
Kama si Babirye kushika nafasi ya tatu, Tanzania ingetawala ulingo wa zawadi kwa ushindi wa 1-2-3.
Nafasi ya nne ilichukuliwa tena na Mtanzania Aalaa Somji mwenye mikwaju 238 wakati nafasi ya tano ilichukuliwa na Mganda Resty Nalutaaya aliyepiga jumla ya mikwaju 240.
Mtanzania Vicky Elias alishika nafasi ya sita kwa kupiga mikwaju 241.
Kulikuwepo na Watanzania saba nchini Uganda katika mashindano ya mwaka huu ya John Walker.
Wengine walioshiriki ni pamoja na katibu wa chama cha gofu ya wanawake nchini TLGU, Yasmin Chali na Loveness Mungure kutoka klabu ya Kili Golf ya Arusha.
Loveness Mungure alimaliza katika nafasi ya 20.