SONGEA United imethibitisha kunasa saini ya Mohamed Badru kuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo atakayeiongoza msimu ujao wa Championship kuisaka tiketi ya Ligi Kuu, 2025/26.
Timu hiyo ambayo awali ilijulikana kama FGA Talents, kwa sasa makazi yake ni mjini Songea na msimu ujao itacheza Championship ikitumia uwanja wa Majimaji mkoani Ruvuma.
Badru aliyewahi kutamba na timu kadhaa hapa nchini ikiwamo Gwambina, Mtibwa Sugar na Azam FC, kabla ya kutua Songea United alikuwa akinoa timu za vijana za Azam.
Meneja wa timu hiyo, Shaban Ibrahim alithibitisha kutua kikosini humo akieleza hadi sasa tayari wameanza mazoezi akibainisha ishu ya usajili wataweka wazi.
“Ni sahihi Badru amesaini kuitumikia timu yetu, yapo baadhi ya mambo mengine tunakamilisha na masuala yote yakiwamo usajili tutaweka wazi baada ya kukamilisha kila kitu,” alisema Ibrahim.
Kwa upande wake Kocha Badru alisema bado mazungumzo yanaendelea na iwapo itakamilika ataeleza kwa undani akiomba kupewa muda hadi watakapofikia makubaliano.
“Kama wao wamethibitisha tusubiri, lakini kwa upande wangu bado sijamalizana nao, ila tusubiri muda kama lipo litakuwa wazi, sina masharti makubwa zaidi,” alisema Kocha huyo.