Rais Samia mgeni rasmi kikao kazi watendaji wakuu wa taasisi

Arusha.  Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kikao kazi cha wenyeviti wa bodi na watendaji wakuu wa taasisi za umma, kitakachofanyika mkoani Arusha.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumapili Agosti 25,2024, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda amesema kikao kazi hicho kitakachofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC) kitafunguliwa Agosti 28,2024 na Rais Samia.

Amesema kikao hicho cha siku tatu kitafunguliwa siku moja baada ya watendaji hao kuanza kukutana Agosti 27, 2024.

“Ni wazi kuwa ugeni huu mzito unakuja na fursa mbalimbali tuendelee kulinda amani, utulivu, upendo, mshikamano ili tuendelee kuhamasisha utalii ikiwemo kuhakikisha Arusha pia inakua kitovu cha mikutano kuanzia ya ndani hadi ya kimataifa,” amesema Makonda.

Kikao kazi hicho kimeandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, kinaongozwa na kauli mbiu isemayo “Mikakati ya Taasisi na Mashirika ya Umma Kuwekeza Nje ya Tanzania”.

Mmoja wa wafanyabiashara jijini Arusha, Joel Kimaro amesema uwepo wa mikutano mikubwa ya ndani na nje ya nchi itasaidia kukuza uchumi kuanzia kwa wafanyabiashara wadogo hadi wakubwa.

“Kiukweli mimi kama mfanyabiashara wa sokoni, uwepo wa mikutano ya mara kwa mara mkoani kwetu inasaidia biashara kuwa nzuri, kwani watu wanakula, kulala na wengine kutumia usafiri, hivyo tunanufaika kwa namna moja ama nyingine,” amesema Kimaro.

Related Posts