TODD: Ule usajili Chelsea, pesa zinatoka huku

LONDON, ENGLAND: CHELSEA inazidi kushusha watu. Usajili kwao wameufanya jambo jepesi sana. Hawamuachi mchezaji wanaomtaka na hadi sasa inafikia idadi ya wachezaji 40 kwenye kikosi hicho.

Wapo 18 waliosajiliwa hadi sasa, huku tisa ikiwa ni kwa kulipa ada na tisa wengine wakiwa ni usajili huru.

Bosi wa miamba hiyo wa Jiji la London, Toddy Boehly kutoa hela ya usajili si tatizo na anachotaka ni kupata kikosi bora cha kuleta mataji, ndio maana usajili wake unahusisha pia kushusha mashine na kumwachia Kocha aangalie nani na nani watamfaa na wengine kuachwa au kutolewa kwa mkopo.

Linapokuja suala la utajiri, Toddy ni mmoja wao na ukitaka kujua anavyopiga pesa, mcheki hapa.

Bosi huyu mmiliki wa Chelsea, anakadiriwa kuwa na utajiri unaofikia Dola 6.1 bilioni na aliinunua Chelsea kwa Pauni 4 bilioni mwaka jana ikiwa ni baada ya kujaribu mara kadhaa na kushindwa.

Anaingiza pesa zake nyingi kutokana na biashara mbalimbali anazofanya na aliwahi kuwa rais wa kampuni ya Guggenheim Partners kabla ya kuachana nayo na kuunda timu ndogo ya watu ambao waliounda kampuni ya Eldridge Industries.

Kampuni hii imejikita zaidi kwenye kuwekeza kwenye sekta mbalimbali za kibiashara pamoja na michezo, pia  imekuwa ikitoa mikopo, kwa mwaka Eldridge inazalisha faida ya zaidi ya Dola 500 bilioni.

Tajiri huyu pia anamiliki hisa za asilimia 20 kwenye timu ya Basseball ya Los Angeles Dodgers ambayo mwaka juzi iliweka rekodi ya kuwa timu iliyolipa kiasi kikubwa cha pesa kwenye mishahara na kodi baada ya kutoa Dola 285 milioni ikiwa ni mara yao ya pili kuweka rekodi hiyo tangu mwaka 2015 walipokuwa na bili ya Dola 291 milioni.

Eldridge iliweka rekodi ya kuingia kwenye orodha ya kampuni zinazotoa mikopo mikubwa zaidi duniani na kwa upande wao imefikia Dola 1 bilioni.

Kipato cha tajiri huyu ndani ya mwaka mmoja kinakadiriwa kuwa ni zaidi ya Dola 200 milioni kutoka kwa vyanzo vyake vya mapato.

Kampuni nyingine ambazo anazimiliki ni pamoja na DraftKings na Esports organisation Cloud9. Pia timu ya kikapu ya Los Angeles Sparks.

Ana nyumba sehemu nyingi ambazo nyingine zimekuwa ni hoteli. Mijengo anayokaa kwa asilimia kubwa ni miwili wa kwanza upo England ambako anaishi sana kipindi hiki kutokana na shughuli zake ndani ya Chelsea, pia ana nyumba Marekani ambako muda mwingi yeye na famili yake ndio wanaishi.

Kijumla nyumba zote anazoishi zinakadiriwa kuwa na thamani ya Dola 50 milioni.

Boehly Family Foundation amekuwa akisaidia jamii kupitia taasisi mbalimbali kama Focused ultrasound Foundation, The Dave Thomas Foundation, Finding a Cure for Epilepsy and Seizures (FACES), The Brunswick School na the Prostate Cancer Foundation.

Kwa mwaka amekuwa akitoa zaidi ya Dola 50 milioni kwa ajili ya kutoa misaada katika taasisi hizi na watu wasiojiweza.

Yupo kwenye ndoa na mrembo Katie Boehly na wamepata watoto watatu, tajiri haonekani sana kwenye fukwe za starehe na muda mwingi amekuwa bize na mambo ya kibishara.

Ana usafiri wa magari makali yenye thamani kubwa na akiwa anafanya safari ya mbali huwa anakwenda na ndege yake binafasi na jumla ya thamani ya vyombo vya usafiri anavyomiliki vinakadiriwa kufikia Dola 20 milioni.

Related Posts