Tuzo yampa jeuri  Mpole | Mwanaspoti

MSHAMBULIAJI wa Pamba Jiji, George Mpole amefunguka kwa mara ya kwanza tangu arejee Ligi Kuu Bara akijiunga na timu hiyo ya Mwanza, akisema tuzo ya Nyota wa Mchezo dhidi ya Dodoma Jiji ni mwanzo wa kazi kubwa aliyojipanga kuifanya msimu huu, licha ya kukataa kujitabiria ufungaji Bora.

Mpole aliyekosa mechi ya kwanza ya msimu huu dhidi ya Tanzania Prisons, juzi alicheza mchezo wa kwanza tangu arejee kutoka FC Lupopo ya DR Congo akipewa dakika 45 zilizotosha kupewa tyuzo ya Mchezaji Bora wa mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Katika mchezo huo, Mpole alifanya majaribio kadhaa dakika ya 47 shuti lake likaokolewa na kipa na kuwa kona, huku dakika ya 71 akigongesha mwamba wa juu baada ya kumchambua kipa, kiwango hicho kizuri kilifanya achaguliwe kuwa mchezaji bora wa mechi na kupewa zawadi na wadhamini wa ligi hiyo.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Mpole aliyekuwa Mfungaji BOra wa 2022-2023 akifunga mabao 17 mbele ya Fiston Mayele wa Yanga aliyemaliza na 16 msimu huo, alisema kwa sasa anazingatia zaidi kuisaidia timu kupata ushindi na kuitoa kwenye presha ya matokeo yasiyoridhisha kuliko kuwaza mafanikio binafsi.

“Siwezi kusema naweza kushindana na mtu, nimekuja kuisaidia timu, timu ikipanda ligi inakuwa na presha kwahiyo sisi tumekuja kuizuia presha ili timu ivune pointi za kutosha ibaki salama. Nashukuru mchezo wangu wa kwanza umekuwa mzuri na umemalizika salama bila majeraha,” alisema Mpole na kuongeza;

“Tuzo inaongeza kitu kikubwa kwangu na inanihamasisha niendelee kupambana nisaidie timu kwa sababu sisi ndiyo lazima tupambane tuwasukume wale ambao bado hawana uzoefu mkubwa,” alisema Mpole

Nyota huyo wa zamani wa Geita Gold, alisema licha ya kuanza kwa sare tasa katika mechi mbili za Ligi Kuu timu yao haijacheza vibaya huku akiwa na matumaini ya kufanya vizuri michezo ijayo kwani timu hiyo iko katika hatua za kutengeneza timu yenye muunganiko na maelewano.

Kocha wa Pamba Jiji, Goran Kopunovic amemwagia sifa Mpole kwa kucheza vizuri baada ya kufanya mazoezi kwa siku 11 na wenzake na kumtaka akiendeleze, huku akionya kwamba hakuna upendeleo ama mchezaji mkubwa bali atakayeoonyesha kiwango kizuri atapangwa.

Related Posts