LIGI Kuu Bara imeanza kwa kusuasua kwa timu nyingi kutoka sare, lakini mastaa wa kigeni wameanza na kasi kwa kufumania mabao wakiwafunika wazawa.
Kabla ya mechi mbili za jana, tayari ilishapigwa michezo saba na kushuhudiwa jumla ya mabao tisa tu yakiwa yametinga wavuni, ikiwa ni idadi ndogo kulinganisha na misimu ya 2022-2023 na 2023-2024 kwa idadi ya mechi kama hizo.
Msimu wa 2022-2023 katika mechi saba kama hizo, jumla ya mabao 17 yalifungwa, wazawa wakiwa 10 dhidi ya wageni watano tu na bao moja la kujifunga, huku kwa msimu uliopita idadi kama hiyo ya michezo yalifungwa 18, wazawa wakiwa tisa na wageni sita tu, pia ikiwamo hat trick moja ya Feisal Salum ‘Fei Toto’.
Kwa msimu huu licha ya Yanga, Azam, KMC, JKT Tanzania na Coastal Union kutocheza mechi hata moja, yamefungwa mabao hayo tisa (kabla ya mechi mbili za jana), wazawa wakifunga mabao matatu, huku wageni wakiwa watano na bao na kipa Daniel Mgore wa Dodoma Jiji likiwa ni la kujifunga.
Wachezaji wa kigeni walianza na mabao hadi sasa ni Mghana Emmanuek Kayekeh, Elvis Rupia raia wa Kenya, Mohamed Diarro (Guinea) na Tra Bi Tra (Ivory Coast) wote wakiichezea Singida Black Stars0, huku Che Fondoh Malone ambaye ni Mcameroon akiifungia Simba katika ushindi wa mabao 3-0 dhidiya Tabora United. Simba jana ilikuwa ikiumana na Fountain Gate, wakati Namungo ilikuwa ikivaana na Tabora.
Nyota wa kizawa walituipia mipra nyavuni kabla ya mechi za jana walikuwa ni Joshua Ibrahim wa KenGold, Valentino Mashaka na Awesu Awesu (wote wa Simba).
Ligi hiyo itaendelea Jumatano wakati Azam FC itaumana na JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Isamuhyo na Alhamisi zitapigwa mechi mbili saa 10 jioni, KMC itavaana na Coastal Union na saa 1 usiku itakuwa zamu ya Yanga itakayokuwa ugenini dhidi ya Kagera Sugar. Yanga, Azam na Coastal zilikuwa kwenye majukumu ya mechi za kimataifa na ligi hiyo itasimama kwa wiki mbili kabla ya kurejea tena Septemba 11.