Rombo. Wananchi waliopo mpakani mwa nchi jirani ya Kenya na Tanzania, katika mipaka ya Holili na Tarakea, iliyopo Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro wameiomba Serikali kutoa elimu ya afya dhidi ya kujikinga na mlipuko wa ugonjwa wa homa ya nyani, maarufu Mpox unaosambaa kwa kasi katika mataifa mbalimbali duniani.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi hao, wameiomba Serikali kutuma jopo la wataalamu katika maeneo mbalimbali wilayani humo, kutoa elimu kwa wananchi namna ya kujikinga na ugonjwa huo kwa kuwa hawana uelewa.
Lina Makyao mkazi wa Kikelelwa, wilayani humo, amesema kwa kuwa ugonjwa huo upo nchi jirani ya Kenya na mwingiliano wa watu kutoka nchi hizo mbili ni mkubwa, elimu inahitajika hasa katika mipaka hiyo, ili wananchi waweze kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo.
“Tunaomba Serikali itume wataalamu wake ipasavyo kuja huku vijijini angalau watoe elimu kwa wananchi dhidi ya ugonjwa huu ambao tayari upo kwa majirani zetu hapa, elimu hii itatusaidia sana maana hatuna uelewa wowote juu ya ugonjwa huu,” amesema Makyao.
Naye, mkazi mwingine wa wilayani humo Lilian Kombe, amesema kwa kuwa hawajui dalili zozote za ugonjwa huo, ananiomba Serikali iendelee kuwaelimisha wananchi wake hasa waliopo maeneo ya mipakani kwa kuwa wao ndio wapo kwenye hatari kubwa zaidi.
“Sisi tuliopo hapa mpakani hatujui hata dalili za huu ugonjwa, hivyo tunaomba Serikali itoe elimu zaidi ili tujikinge japo haujaingia nchini kwetu, tunasikia kuwa idadi ya wagonjwa katika maeneo mengi inazidi kuongezeka,” amesema Kombe.
Sakima Mosha, mkazi wa Keni wilayani humo amesema endapo kinga dhidi ya ugonjwa huo itapatikana mapema itakuwa salama kwao, kwa kuwa mwingiliano wa nchi hizo mbili ni mkubwa hasa mipaka ya Tarakea na Holili.
“Tunaomba tupatiwe kinga ya homa ya nyani, maana wenzetu hapa jirani ambao tayari ugonjwa huu umefika kwao, wanaingia na kutoka hapa kwetu na sisi vivyo hivyo, lakini tungepata kinga ingeweza kutusaidia zaidi,” amesema mwananchi huyo.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Katangara Mrere, wilayani humo Mallel Venancy amewaomba wataalamu wa afya waliopo kwenye kata hiyo kuendelea kutoa elimu kwa wananchi wa kata hiyo namna ya kujikinga.
Akizungumzia tahadhari walizozichukua, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amewaomba wananchi kuendelea kuchukua tahadhari juu ya ugonjwa huo na kufuata maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya.
“Tumepeleka maelekezo kwenye mipaka yetu yote wa Holili na Tarakea na maeneo mengine, kwa hiyo naomba tuchukue tahadhari kubwa kuhakikisha tunafuata maelekezo yanayotolewa na wataalamu wetu wa afya, ambao wameendelea kutoa maelekezo juu ya ugonjwa huu,” amesema Babu.