DC ajitosa kumsaidia mwanafunzi aliyeacha shule alee wadogo zake

Njombe. Siku moja baada ya Mwananchi kuripoti taarifa kuhusu Sarah Chaula (17), mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Ilumaki, wilayani Makete Mkoa wa Njombe, aliyeacha masomo ili awalee wadogo zake wawili, Nuru Chaula (13) na Faraja Chaula (10), hatimaye Serikali ya Wilaya ya Makete imeingilia kati.

Mtoto huyo mkazi wa Kijiji cha Ugabwa, alilazimika kufanya hivyo baada ya wazazi wake kuondoka nyumbani kwa sababu tofauti, ikiwamo ya baba kutofautiana na mama na baadaye mama kukimbia kutokana na deni la Sh2 milioni linalodaiwa kusababishwa na mtoto wao wa kiume.

Hivyo, Serikali imechukua hatua za kumrejesha Chaula shuleni aendelee na masomo yake katika shule hiyo.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu Agosti 26, 2024 kwa simu, Mkuu wa Wilaya ya Makete, Juma Sweda amesema ofisi yake haikuwa na taarifa juu ya mwanafunzi huyo kuacha masomo.

Amesema wiki tatu zilizopita alifanya mkutano wa hadhara kwenye Kijiji cha Ugabwa, lakini hoja hiyo haikuibuliwa na wananchi, licha ya mkutano kufanyika kwa zaidi ya saa tatu.

Sweda amesema baada ya taarifa hizo kuripotiwa jana, alishangaa na aliamua kuwatuma viongozi kutoka ofisi ya ustawi wa jamii ya wilaya waende wakajiridhishe na taarifa hizo.

“Wamefika na kweli wamewakuta wale watoto na inavyoonekana wale watoto walikuwa wanalelewa na upande wa mama na yeye ndiyo alikuwa mlezi mkubwa, lakini baadaye mama yule alitoroka pale nyumbani baada ya deni hilo la mtoto wake wa kiume, yule mama alikuwa mdhamini,” amesema Sweda.

Amesema deni hilo liliripotiwa polisi, kutokana na hofu mama huyo alikimbia na kuwatelekeza watoto wake hao, akiwamo Sarah Chaula.

Hivyo, amesema hatua ambazo tayari Serikali ya wilaya imeanza nayo ni ya kumrejesha shuleni mwanafunzi huyo pale alipokuwa akisoma.

Sweda amesema ametoa maelekezo kwa mkuu wa shule hiyo, wamsaidie kwa kutenga muda maalumu wa kumfundisha, ili aende sawa na wenzake kipindi ambacho hakuwepo shuleni.

“Wale watoto wengine wawili nao wamerudishwa shule. Mmoja Bulongwa mwingine tumemrudisha shule aliyokuwa anasoma, kifupi wote wamerudi shuleni,” amesema mkuu huyo wa wilaya.

Amesema hatua nyingine iliyochukuliwa na Serikali ni kumtafuta mtu anayedaiwa kuidai familia hiyo na kusababisha mama huyo kukimbia na amepatikana na amekiri kuidai familia hiyo.

Ili kulitatua hilo, Sweda amesema amepanga kukutana na mtu huyo ofisini kwake, lengo likiwa kwanza kuhakiki deni hilo na baadaye waangalie uwezekano wa kuisaidia familia hiyo kulilipa deni hilo, kusudi huyo mama arejee nyumbani kwake kuwalea watoto wake.

Hata hivyo, ametoa tahadhari kwa wananchi wengine wilayani humo, wanapokopa wasikimbie familia zao, badala yake wafike kwenye ofisi za Serikali kusaidiwa.

Awali, Chaula aliiambia Mwananchi kuwa sababu ya kuacha masomo ilikuwa ni kuwatunza wadogo zake wawili baada ya wazazi wao kuwatelekeza na kutokomea kusikojulikana.

Alisema mama yake alikimbia deni la Sh2 milioni liliosababishwa na kaka yao ambaye naye amtokomea kusikojulikana.