Mtazamo hasi chanzo wanafunzi kukimbia hisabati

Moshi. Wakati wanafunzi wengi hususani wa kike wakitajwa kulikimbia somo la hisabati kwa madai kuwa ni gumu, mtazamo hasi juu ya somo hilo ndani ya jamii, umetajwa kuwa moja ya sababu za wanafunzi kuliogopa somo hilo.

Hayo yamesemwa leo Jumatatu Agosti 26, 25024 na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Eden Garden, Samuel Solomon wakati wa uzinduzi wa programu ya elimu kwa vitendo inayohusisha masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi, sanaa na hisabati (Steam) shuleni hapo kwa lengo la kukuza vipaji.

Mwalimu Solomon amesema pia baadhi ya walimu wamekuwa wakiwajengea wanafunzi mtazamo hasi kuwa somo la hisabati kuwa ni gumu, jambo alilosema huwafanya wanafunzi kukata tamaa na kuchukia somo hilo.

“Kupenda ama kutokupenda somo la hisabati kunaanza na mazingira halisi aliyopo mtoto na katika jamii nyingi husema somo la hisabati ni gumu, hii huwajengea watoto mtazamo hasi kuwa hawataliweza somo hili na kuwafanya wengi kulichukia.

“Hisabati haifanyi vizuri kwa sababu huko mwanzo hata walimu wa somo hilo walianza kutumia lugha hasi kwa wanafunzi, jambo lililowafanya wengi kuona ni kitu ambacho hakiwezekani,” amesema Mwalimu Solomon.

Amesema wanafunzi wanapaswa kujua kuwa hisabati inatumika katika maisha ya kila siku, hivyo ni muhimu kubadili mtazamo wa jamii kuhusu somo hilo.

Akizungumzia programu ya Steam, Solomon amesema ni moja ya mapokeo ya maboresho ya mtalaa wa elimu nchini ambao unataka kumuandaa mwanafunzi kwa ajili ya stadi za maisha za karne ya 21, ili baadaye wawe washindani katika soko la ajira, biashara na fursa zote zitakazojitokeza kwao.

Mkurugenzi mtendaji wa shule za Eden Garden, Patricia Kombe amesema programu ya Steam itawezesha wanafunzi kusoma kwa vitendo na kupata mbinu za kuendana na dunia ya sasa ya sayansi na teknolojia.

“Programu hii inaandaa vijana bora wa baadaye, ili wajifunze kwa vitendo na kuwa wabunifu, wadadisi, kujiamini na kukuza ujuzi na kutatua changamoto za karne ya 21,” amesema.

Ametoa wito kwa wazazi na jamii kuhakikisha watoto wao wanaingia katika programu hiyo, kwani itawasaidia watoto kukuza vipaji na kufanikiwa kwa chochote wanachotaka maishani, hivyo kukabili changamoto za karne ya 21.

“Karne ya 21 inahitaji vijana au watu wanaoweza kutatua changamoto, inahitaji watu wanaoweza kutumia teknolojia, hivyo watoto wetu wasipojifunza teknolojia wataachwa nyuma,” amesema.

Akizungumza katika uzinduzi huo, mmoja wa wazazi, Peter Kileo amesema programu ya steam ni nzuri kwa kuwa inawaandaa wanafunzi kushindana katika ulimwengu wa sayansi na teknolojia na kuiomba Serikali kuona uwezekano wa shule zote, zikiwemo za Serikali kuitumia.

Baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo, wamepongeza uanzishwaji wa programu hiyo na kueleza itawaandaa kuwa hodari, imara na kuwawezesha kutimiza ndoto zao za baadaye.

“Programu hii imeletwa kwa ajili ya kutuwezesha kufika mbali katika stadi za maisha, naomba shule nyingine watumie programu hii ili kuwezesha wanafunzi kujifunza kwa vitendo na kutambua vipaji vyao wangali wadogo na hatimaje watimize ndoto zao hapo baadaye,” amesema Sabra Izadin, mwanafunzi wa darasa la nne.

Kwa upande wake, Alia Omary amesema wanafunzi wengi wa kike hawapendi kusoma hisabati kwa sababu wanaona ni somo ngumu na hawataki kuchoka na kushauri wanafunzi wenzake kuondokana na mtazamo huo.