Sadala matumaini kibao Biashara Utd

NYOTA mpya wa Biashara United ya Mara, Sadala Lipangile ambaye amesajiliwa akitokea KMC amepania kutumia uzoefu alionao kuwa sehemu ya historia ya chama hilo kurejea Ligi Kuu Bara.

Msimu uliopita Biashara ilisaliwa na hatua moja tu kurejea Ligi Kuu lakini ilijikuta wakikwaa kisiki mbele ya Tabora United katika hatua ya mchujo baada ya kupoteza kwa jumla ya mabao 2-1.

Sadala anaamini Biashara inauwezo wa kurejea Ligi Kuu na ndio maana kwake haikuwa ngumu kukubali ofa aliyopewa na mabosi wa timu hiyo; “Biashara wana mipango mizuri na mikubwa hivyo sina shaka na uamuzi nilioufanya.

“Nilikuwa na nafasi ya kuendelea kucheza Ligi Kuu lakini nikaona siyo mbaya kukabiliana na changamoto ya soka la Championship, najua ni ligi ngumu ila nipo tayari kwa maisha hayo mapya,” alisema mchezaji huyo ambaye pia aliwahi kuichezea Mbao FC.

Wakati akiwa KMC, Sadala alikuwa kivutio kwa wengi kutokana na uwezo alionao wa kucheza zaidi ya nafasi moja uwanjani, kipo kipindi alitumika kama beki wa kati na hata mshambuliaji wa mwisho na kuwa msaada katika upachikaji mabao.

Akiwa Biashara, Sadala ataungana na kipa David Kissu ambaye aliwahi kucheza naye kikosi kimoja wakati akiwa KMC. Kwa sasa Biashara inaendelea na maandalizi yake huko Mara kwa kucheza michezo ya kirafiki huku wakisubiri msimu mpya wa Championship kuanza mwezi ujao, Oktoba.

Biashara United ilianzishwa 1990 ikifahamika kama Police Mara kabla ya kubadilishwa jina hilo 2013. Chama hilo lilipanda Ligi Kuu Bara msimu wa 2018/19 na 2020/21 lilimaliza ligi likiwa nafasi nne za juu na kushiriki michuano ya kimataifa kabla ya 2021/22  kushuka daraja.