USHINDI wa mabao 2-1 ilioupata Tabora United juzi katika Ligi Kuu Bara dhidi ya Namungo FC, umeifanya kuvunja mwiko wa kutoshinda ugenini tangu ipande daraja 2022-2023, baada ya kucheza michezo 17.
Mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Majaliwa, Lindi, Namungo ilipata bao kupitia kwa Djuma Shabani kwa penalti dakika ya 60 huku Tabora ikisawazisha kwa penalti ya Heritier Makambo dakika ya 72 na Salum Chuku akitupia la pili dakika ya 90.
Kabla ya ushindi huo, Tabora United ilikuwa haijawahi kushinda ugenini katika Ligi Kuu Bara ambapo kwa msimu uliopita na huu imecheza michezo 17, na kati ya hiyo imeshinda mmoja, sare mitano na kuchapwa 11.
Katika michezo 17 ya ugenini iliyocheza msimu uliopita hadi huu wa sasa, imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara 30, huku eneo la ushambuliaji ambalo linaongozwa na Makambo msimu huu likifunga mabao tisa. Makambo amerudi nchini kwa mara ya tatu baada ya kuichezea Yanga kwa misimu tofauti na kuteka mashabiki na aina yake ya ushangiliaji ya kuwajaza, huku akibeba imani kubwa ndani ya timu hiyo katika eneo la ushambuliaji kutokana na uzoefu wake.
Kwa mara ya kwanza Makambo alitua nchini Julai Mosi, 2018 akitokea FC Lupopo ya kwao Congo na kuitumikia hadi Agosti 10, 2019 na kujiunga na Horoya AC ya Guinea na kuichezea misimu miwili kisha kurejea tena Yanga na kuondoka Januari 2023.
Nyota huyo ambaye ni mchezo wake wa kwanza dhidi ya Namungo msimu huu, ameanza kuonyesha makali yake baada ya kuhusika na mabao yote mawili ya Tabora kufuatia kufunga moja kisha kutoa pasi ya bao la ushindi lililofungwa na Salum Chuku.
Msimu wake bora kwa nyota huyo ni ule wa kwanza akiwa na Yanga wakati anatokea FC Lupopo ya kwao Congo alipofunga jumla ya mabao 21 katika mashindano mbalimbali ambapo 17, yalikuwa ni ya Ligi Kuu Bara huku manne ni ya Kombe la Shirikisho la FA.
Kocha mkuu wa timu hiyo Francis Kimanzi alisema amefurahishwa na kurejea kwa wachezaji wote hasa wale wa kigeni ambao walikosa vibali na kusababisha kuukosa mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Bara waliopoteza kwa mabao 3-0 dhidi ya Simba Agosti 18.
“Haikuwa rahisi kwa sababu ni mchezo wa pili kwetu ugenini msimu huu ila tunashukuru tumepata pointi tatu muhimu baada ya kuzikosa mechi ya kwanza, ushindani ni mkubwa sana hivyo tunaendelea kupambana ili kutengeneza timu imara,” alisema.
Kimanzi aliyezaliwa Mei 29, 1976, amejiunga na kikosi hicho msimu huu huku akiwa na rekodi kubwa ya kuzifundisha timu mbalimbali za Kenya ikiwemo ya taifa ‘Harambee Stars’, na klabu zikiwemo za Wazito, Mathare United, Sofapaka na Tusker FC.