Tume yataja idadi watakaoandikishwa daftari la kudumu Mkoa wa Mara

Musoma. Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) inatarajia kuandikisha wapigakura wapya 199,501 katika Mkoa wa Mara wakati wa uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura.

Idadi hiyo ni sawa na ongezeko la asilimia 17 la wapigakura 1,115,777 waliopo katika daftari hilo kwa Mkoa wa Mara.

Akizungumza mjini hapa jana Jumapili Agosti 25, 2024 kwenye kikao kati ya tume hiyo na wadau wa uchaguzi mkoani Mara, mkurugenzi wa tume hiyo, Ramadhani Kailima amesema uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura kwa mkoa wa Mara unatarajiwa kuanza Septemba 4 hadi 10 mwaka huu.

Kailima amewaomba wadau hao kila mmoja kwa nafasi yake kuwahamasisha wadau wake wenye sifa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha, ili wapate nafasi ya kushiriki kwenye uchaguzi mkuu ujao kwa kupiga kura na kuwachagua viongozi wanaowataka.

“Mfano ndugu zangu viongozi wa dini mna nafasi ya kutumia taasisi zenu, nyumba zenu za ibada kuwahamasisha waumini na waamini wenu wale wenye sifa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na wale wenye kurekebisha taarifa zao pia watumie fursa hiyo ya siku saba kufanya hivyo,” amesema Kailima.

Amesema uboreshaji huo utawahusu wale ambao hawajawahi kuandikishwa kwenye dafari hilo pamoja na wanaotaka kubadilisha taarifa zao kutokana  na sababu mbalimbali, ikiwemo kuhama kutoka katika maeneo  ya awali waliyoandikishwa, waliopoteza  kadi zao au sababu nyingine kwa mujibu wa sheria taratibu na kanuni.

Amefafanua kuwa uboreshaji huo hautawahusu wale wenye kadi zilizotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kati ya mwaka 2015 na 2020 kwa maelezo kuwa kadi hizo ni halali na zinatambuliwa na INEC.

“Kwa mtu mwenye kadi ya NEC iliyotolewa  kati ya mwaka 2015 na 2020 na hana shida yoyote ile, mfano hajahama makazi wala kupoteza kadi yake asihangaike, kwani kadi hizo ni halali na zitatumika kwenye uchaguzi ujao bila kikwazo chochote,” amesema.

Awali, akifungua kikao hicho, mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji mstaafu Jacobs Mwambegele amewataka wakazi wa Mkoa wa Mara kuzingatia sheria, kanuni na taratibu wakati wa kuboresha taarifa zao, ili kuepuka kuchukuliwa hatua za kisheria pale watakapokwenda kinyume.

“Kuna wengine wanajaribu kujiandikisha zaidi ya mara moja, hawa wanataka kujaribu mfumo wa tume upoje, naomba wasijaribu kwani sheria iko wazi ukifanya hivyo zipo adhabu kali zitachukuliwa juu yako ikiwa ni pamoja na kifungo jela,” amesema.

Baadhi ya wadau walioshiriki kikao hicho wamesema ili tume hiyo itende haki na mchakato wote wa uchaguzi kuwa huru na haki, ni vema vyama vyote vinavyoshiriki vipewe fursa sawa bila upendeleo au ubaguzi.

“Hawa wasimamizi wenu wanaotumia kigezo cha wagombea wa vyama vingine kutokujua kusoma na kuandika kama pingamizi mbali na kuminya uhuru wa vyama hivyo, lakini pia wanalitia aibu Taifa kwa kudai kuwa wagombea wengi hawajui kusoma na kuandika kitu ambacho kwanza hakina ukweli,” amesema Christina Ndengo.

Anastazia Marwa amesema ushirikishwaji wa makundi yote ya kijamii yakiwepo makundi maalumu, ni jambo la muhimu kufanikisha malengo hayo ya tume, hali ambayo pia itawapa haki na fursa sawa kushiriki kwenye uchaguzi mkuu.

Amesema kundi la watu wenye ulemavu hasa wasioona, bado halijapewa fursa sahihi katika mchakato wote wa uchaguzi kuanzia uandikishwaji, kushiriki kampeni na hata upigaji kura, hivyo ni matarajio yao kuwa kwa mwaka huu kundi hilo litapewa fursa na kipaumbele ili washiriki kikamilifu kama ilivyo kwa watu wengine.

Related Posts