Morogoro. Jeshi la Polisi mkoani Morogoro linafuatilia taarifa za baadhi ya wahalifu kutumia mavazi aina ya kanzu na majuba kufanya uhalifu hasa asubuhi.
Hayo yameelezwa na kamanda wa polisi mkoa huo, Alex Mkama leo Jumatatu Agosti 26, 2024 alipozungumza na Mwananchi, akisema tayari wana taarifa za aina mpya ya uhalifu huo na wanazifanyia kazi.
“Hizi taarifa za vibaka kutumia mbinu ya kuvaa kanzu na majuba ndio nimezipokea na nitazifanyia kazi haraka iwezekanavyo, sisi polisi tunafanyia kazi taarifa yoyote inayotufikia na kwenye hili tutaomba wananchi watupe ushirikiano,” amesema Mkama.
Amesema changamoto kubwa wanayoipata polisi katika kushughulikia taarifa hizo ni kukosekana kwa ushirikiano wa wananchi pamoja na kushindwa kutoa ushahidi kesi hizo zinapofikishwa mahakamani.
“Tukipewa taarifa sisi polisi tunafanyia kazi, lakini tukishafikisha kesi mahakamani wahusika wa kutoa ushahidi hawaonekani, sasa Mahakama inashindwa kuwatia hatiani na hivyo inabidi waachiwe. Wakirudi mtaani wananchi wanaanza kulinyooshea vidole jeshi la polisi,” amesema Mkama.
Taarifa za kutokea uhalifu kwa njia hiyo zimetajwa katika maeneo ya Mafisa, Kichangani, Mjimpya, Vibandani, Chamwino, Mbuyuni na Azimio na Kilolo.
Akizungumzia uhalifu huo, Mwenyekiti wa Mtaa wa Bambalawe Kata ya Mbuyuni, Kelvin Banzi amesema matukio hayo ya uporaji yamekuwa wakitokea alfajiri, wakati wananchi wanawahi kwenye shughuli zao za kila siku na usiku kuanzia saa tatu hadi sasa tano.
“Hii kata imepakana na SUA (Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine) na wanafunzi wengi wamekuwa wakipanga huku, sasa inapofika saa 3 mpaka saa 5 usiku wanafunzi wanakuwa wametoka kujisomea chuo na wao ndio waathirika wakubwa wa matukio haya,” amesema Banzi.
Amesema vitendo hivyo vya uporaji vimekuwa vikifanywa na vijana wanaoishi maeneo hayo, lakini wananchi wanaogopa kuwataja kwa polisi kwa kuhofia taarifa hizo kuvuja na kuwarudia vibaka hao na baadaye kutengeneza visasi.
“Polisi ni kweli wanakuja mtaani wanawakamata, lakini siku mbili wote waliokamatwa wanaonekana tena mtaa tena.
“Baya zaidi vibaka hawa wamekuwa pia wakivuta bangi na wakitumia silaha kama mapanga, nondo, visu na bisibisi na wamekuwa wakivaa kanzu na wengine majuba wakijifanya wanakwenda msikitini, Kwa kweli wananchi wamekuwa na hofu kubwa kutokana na matukio yaliyotokea,” amesema.
Kwa upande wake, diwani wa Mbuyuni, Samwel Msuya amesema kwa kiasi kikubwa kata hiyo inasumbuliwa na matukio ya ukabaji na uporaji ambayo yamekuwa yakifanywa na vijana wenye umri mdogo ambao wengine wameacha shule.
“Kinachosababisha watu wanaoporwa kushindwa kutoa taarifa ni kutokana na kutokuwepo kwa uhakika wa kupatikana kwa mali zao kama simu na kompyuta mpakato.
“Mtu anaibiwa, akienda kutoa taarifa polisi kinachofuata ni usumbufu wa njoo kesho, njoo kesho kutwa, ndio maana sasa hivi mtu akiporwa basi anamwachia Mungu na kuamua kutafuta simu nyingine,” amesema Msuya.