Arusha. Hongo, zawadi ndogondogo pamoja na mmomonyoko wa maadili zimetajwa kuwa chanzo cha matukio ya ukatili wa kingono kwa wanafunzi shuleni.
Kutokana na hilo, wazazi na walezi wametakiwa kuongeza ukaribu na watoto wao katika malezi, lakini pia Serikali iongeze adhabu kwa watu wanaothibitika kutenda makosa ya kinyume na maadili, hasa ubakaji na ulawiti wa watoto.
Hayo yamesemwa leo Jumatatu Agosti 26,2024 jijini Arusha na Mwalimu Joyce Munisi wa Shule ya Msingi Moshono kwenye semina ya walimu walezi wa klabu za maadili, iliyoratibiwa na Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili kwa Viongozi wa Umma kwa lengo la kujadili mikakati ya kutokomeza mmomonyoko wa maadili kwa wanafunzi wao.
Mwalimu Joyce amesema asilimia kubwa ya matukio ya ukatili yanayoendelea nchini yanasababishwa na mmomonyoko wa maadili kwenye jamii, lakini pia wanaotendewa baadhi yao hurubuniwa na zawadi ndogondogo kama fedha na vitu vya kula.
“Sasa hivi tumekuwa tukisikia baba mtu mzima amebaka au amemlawiti mtoto mdogo mwenye umri sawa na mwanaye, lakini wengine wanafikia hadi kuwarubuni watoto wao. Huu ni ukatili mbaya, sababu kubwa ni mmomonyoko wa maadili.
“Mbali na hiyo, watoto wengine tumekuwa tukiwafundisha namna ya kuepuka vitendo hivyo kwa kutoa taarifa anapoona dalili za kutendewa, lakini wengine wanakwenda wenyewe kwa kudanganywa na vizawadi vidogovidogo ambavyo havina maana hadi anakuwa mtumwa wa ubakaji au ulawiti,” amesema Mwalimu Joyce.
Amesema kuwa bado jamii ina kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha inarejesha heshima yake ya zamani, hasa ya kimaadili.
“Serikali nayo kupitia vyombo vya sheria iangalie namna ya kushughulika na kesi hizi, ikiwemo kuziharakisha. Pia iongeze adhabu za wanaotekeleza matukio haya ili kuyatokomeza,” amesema Mwalimu Joyce.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Katibu Msaidizi, Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Kanda ya Kaskazini, Gerald Mwaitebele amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwanoa walimu walezi wa klabu za maadili kufahamu mwongozo wa kuanzisha na kulea klabu hizo, hasa mbinu, mikakati ya kukabiliana na mmomonyoko wa maadili.
Amesema lengo la kuitisha semina hiyo ni baada ya kuona vitendo vya mmomonyoko wa maadili vinashamiri, hivyo kuhatarisha ustawi wa Taifa baadaye hasa katika upatikanaji wa viongozi na watumishi wa umma wenye maadili na uzalendo.
“Siku hizi tumekuwa na wakati mgumu dhidi ya janga la mmomonyoko wa maadili kwenye jamii, hasa zinazoletwa na tamaduni za nje ambazo inaharibu vijana kwa kiwango kikubwa, ndio maana leo tuko hapa kuwanoa walimu walee vema watoto hawa shuleni.
“Waazazi nao waangalie namna wanavyoishi na watoto wao hasa katika kuwaepusha na vitendo vya ukatili,” amesema Mwaitebele.
Awali akifungua mafunzo hayo, Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Missaile Mussa aliwataka walimu kuzingatia elimu wanayopewa na kujiepusha na vitendo visivyo vya kimaadili kwenye maeneo yao ya kazi, jamii na kwa wanafunzi wao.
Aliwataka wazazi kuwa karibu na watoto wao katika malezi na kuzungumza nao mara kwa mara kirafiki juu ya matukio ya ukatili, ili kuwaepusha na vitendo hivyo.
“Wazazi wawe wanajitathimini wanaishije na watoto wao na wanaona nini kutoka kwao ili wasije kujikuta wao ndio chanzo cha mmomonyoko wa maadili yanayoendelea kwenye jamii, kwani inazidi kuliweka hatarini Taifa letu baadaye” amesema Misaile.