CCM: Dk Nchimbi hakuthibitisha kushiriki mdahalo wa Odemba

Dar es Salaam. Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema Katibu Mkuu wake, Dk Emmanuel Nchimbi hakukimbia mdahalo kama ilivyoelezwa na mtangazaji, badala yake hakukuwa na mawasiliano rasmi ya kumwalika.

Kwa mujibu wa taarifa ya CCM, hadi matangazo ya kufanyika mdahalo huo yanasambazwa mitandaoni, Dk Nchimbi hakuwa amethibitisha kushiriki wala kuahidi kutuma mwakilishi na tayari alishamshauri mwandaaji njia sahihi ya kumwalika.

Kauli hiyo ya CCM inajibu madai ya mtangazaji wa kipindi cha Medani za Siasa, Edwin Odemba kinachorushwa na kituo cha luninga cha Star TV kuwa, kutofanyika kwa mdahalo huo, kumesababishwa na Dk Nchimbi kutotokea.

Mzizi wa yote hayo ni mdahalo uliopangwa kufanywa na Star TV ukihusisha makatibu wakuu wa vyama vitano vya siasa nchini ambavyo ni CCM, Chadema, CUF, NCCR Mageuzi na ACT-Wazalendo.

Lakini, siku ya mdahalo huo uliopangwa kufanyika katika Ukumbi wa Maktaba Kuu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ilifika na watendaji wakuu wa vyama vingine walikuwepo, isipokuwa Dk Nchimbi na Ahmed Masoud wa CUF.

Baada ya mazingira hayo, Odemba alifungua kipindi hicho na kutangaza mdahalo wa viongozi hao hautafanyika kwa kuwa Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika amesema hatashiriki kama Dk Nchimbi hayupo.

Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu naye alidai hatoshiriki kwa sababu Mnyika amekataa kushiriki, kwa mujibu wa Odemba aliyezungumza mbele ya luninga huku akibubujikwa machozi.

Katika mazingira hayo, Odemba alitangaza kutofanyika kwa mdahalo huo, badala yake mada zilizopangwa zilijadiliwa na wahudhuriaji wengine na kwa sehemu kubwa walimtupia lawama Dk Nchimbi kwa kutoshiriki.

Kutokana na lawama hizo, CCM katika taarifa yake iliyotolewa leo Jumapili, Septemba 1, 2024 iliyotiwa saini na Katibu wa Dk Nchimbi, Dennis Msacky ilieleza kusikitishwa na kauli ya Odemba katika kipindi hicho.

“CCM inautaarifu umma kuwa Katibu Mkuu hakukimbia wala hakudharau mdahalo huo. Balozi Nchimbi alifanya kila jitihada za mawasiliano na mwandaaji na tunasikitishwa na jinsi alivyoupotosha umma,” imesema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa Agosti 10, 2024 Odemba alimtafuta Dk Nchimbi kwa kutuma ujumbe mfupi wa maandishi (sms) akimuomba ashiriki mdahalo huo wa viongozi wa vyama vya siasa.

“Katibu Mkuu alimjulisha kuwa masuala ya vyombo vya habari yanaratibiwa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla hivyo awasiliane naye na akampa namba ya simu ya mkononi ya Makalla,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Amesema kwa sababu ambazo Odemba anaweza kuzieleza mwenyewe, katika kipindi cha takriban wiki tatu, hakufanya mawasiliano au kumtafuta Makalla kama alivyoelekezwa na kushauriwa na Dk Nchimbi.

“Baada ya kuhisi kwamba nafasi ya Katibu Mkuu inaweza kuwa ngumu kupatikana kutokana na majukumu yake ya kazi za chama, Odemba alimtafuta tena Balozi Nchimbi akiomba amuandae mwakilishi huku matangazo ya mdahalo huo yakiendelea kumtaja Katibu Mkuu wa CCM kuwa ndiye atakayeshiriki,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Taarifa imeeleza kuwa badala yake Katibu Mkuu alimwelekeza Odemba kutofanya lolote kabla ya kupata mawasiliano na Sekretarieti ya CCM.

“Kimsingi Odemba alitaka wananchi wadanganywe kuwa CCM kupitia kwa Katibu Mkuu ilikuwa imethibitisha kushiriki katika mdahalo huo jambo ambalo si sahihi.

“Katika mazingira ya kustaajabisha tumeshangazwa na machozi ya Odemba aliyotoa jana akielekeza lawama kwa CCM na kwa Katibu Mkuu, wakati alijua bayana kwamba alikuwa hajapata uthibitisho wowote wa CCM kushiriki.”

“Ikiwa ni pamoja na ukweli kwamba yeye mwenyewe alishajua kwamba alikuwa akiendelea kutangaza kuhusu mdahalo huo kama ‘promo’ pasipo kupata ridhaa ya CCM,” imesema.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Katibu Mkuu wa CCM ndiye Mwenyekiti wa Sekretarieti na siku nzima ya jana ambayo ndiyo siku Odemba alipanga kufanyika kwa mdahalo huo, kulikuwa na vikao vya maandalizi ya Kamati Kuu Maalumu ambayo inafanyika leo.

“Jambo ambalo kwa namna yoyote Katibu Mkuu asingeweza kuwapo katika mdahalo huo hata kama angekuwa amethibitisha awali. Kushiriki kwenye mdahalo kunahitaji mashauriano na maafikiano kati ya waandaaji na waalikwa,” imeeleza.

Imesema Katibu Mkuu hakuwa ametoa uthibitisho wa kuhudhuria mdahalo huo na hakukuwa na makubaliano yoyote rasmi ya yeye au mwakilishi wake kuhudhuria katika shughuli hiyo.

“Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Nchimbi yupo tayari kwa midahalo, majadiliano na makongamano yanayolenga kujenga umoja wa kitaifa na maridhiano ya kisiasa kadiri ya taratibu zilizopo na ratiba yake ya kazi inavyoruhusu,” imeeleza taarifa hiyo.

Related Posts