Latra yafanya mabadiliko mfumo wa uendeshaji wa usafiri wa umma

Arusha. Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra) imebadilisha mfumo wa utoaji wa huduma za usafiri wa umma kutoka mtu mmoja mmoja (binafsi) na sasa inatarajia kuanza kuendeshwa na jumuiya ya watu wanaounda ushirika au kampuni.

Mfumo huo unaowataka wamiliki wa vyombo vya usafirishaji kuunda jumuiya, ushirika au kampuni, una lengo la kuwapa wadau hao mamlaka ya kujisimamia wenyewe katika uendeshaji pia kuwapatia fursa za uwekezaji.

“Utaratibu huu utawaunganisha watoa huduma za usafiri wa umma kwenye mfumo jumuishi wa utoaji huduma kama ushirika, Saccos au kampuni,” amesema Kaimu Mkurugenzi wa Barabara kutoka Latra, Leo Ngowi wakati akitoa elimu juu ya mfumo huo mpya unaotarajiwa kuanza kutumika mwakani.

Semina hiyo ya siku moja imehudhuriwa na wamiliki wa vyombo vya usafiri wa umma Kanda ya Kaskazini pamoja na viongozi wa vyama vya madereva wa mabasi, daladala, pikipiki za magurudumu matatu na mawili.

Ngowi amesema mfumo huo utasaidia wahusika wa sekta ya usafirishaji kutoa huduma bora, salama, rahisi na rafiki kwa mazingira kwa ajili ya kuvutia watu wengi zaidi kutumia usafiri wa umma.

“Pia mfumo huu utaweka mazingira wezeshi ya uwekezaji kwa huduma bora ambao wahusika wataweza kuwekeza na kumudu soko la ushindani. Pia itawapa nguvu na uwezo wa kusimamia huduma za usafiri hasa mijini” amesema Ngowi.

Akizungumzia Mfumo huo, Katibu wa Chama cha Wasafirishaji wa abiria Mkoa wa Arusha na Kilimanjaro (Akiboa), Adolf Locken aliiomba serikali kuweka mda wa kutosha kupitisha mfumo huo kuwa sheria rasmi za Latra, ili kuruhusu wamiliki waliopo kuelewa na kutoa huduma itakayoendana na mabadiliko hayo.

“Lakini pia watusaidie kutuunganisha na taasisi ya kifedha na ikiwezekana wawe sehemu ya wadhamini wetu ambao itaongeza thamani ya mkopo na uharaka ili kuweza kuendana na mabadiliko ya mfumo,” amesema Locken.

Katibu wa umoja wa waendesha bodaboda jiji la Arusha, Hakimu Msemo alisema kuwa mfumo huo unaweza kuwa rafiki pale watakapopata elimu ya kutosha juu ya mfumo na jinsi utakavyoweza kuwanufaisha.

Akifungua mafunzo hayo, Katibu Tawala Mkoa wa Arusha Missaile Mussa amesema kuwa sekta ya usafirishaji mbali na umuhimu wao katika utoaji wa huduma pia imekuwa na mchango mkubwa kiuchumi.

“Usafirishaji ni moja ya sekta kubwa ya binafsi inayochangia ukuaji wa uchumi wa nchi yetu hivyo tumieni fursa hii kuendana na mabadiliko hayo kwa manufaa yenu kiuchumi na Serikali kwa ujumla,” amesema Mussa.

Mbali na hilo aliwataka wadau hao kuepuka ajali za mara kwa mara lakini pia matendo na matukio ya mmomonyoko wa maadili yanayoendelea kwenye jamii bali watangulize uzalendo kwa kila jambo wanalotaka kufanya mitaani ili kuisaidia nchi kuendelea kuwa salama na amani kwa ustawi wa shughuli zao.

Related Posts