Chalamanda alia dakika za lala salama

KIPA wa Kagera Sugar, Ramadhan Chalamanda amesema kupoteza umakini katika dakika za mwisho ndiko kumewanyima pointi sita katika michezo miwili waliyocheza, huku akiahidi mchezo dhidi ya Tabora United kitaeleweka.

Kagera Sugar ambayo haijawahi kushuka daraja tangu ilipopanda Ligi Kuu Bara 2004, msimu huu haijaanza na matokeo mazuri ikipoteza michezo miwili mfululizo na kuwa mkiani kwenye msimamo.

Timu hiyo pekee ya Ligi Kuu kutoka mkoani Kagera ilianza kwa kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Singida Black Stars kisha ikalala mabao 2-0 mbele ya Yanga, mechi zote zikipigwa katika Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

Lakini sasa itakuwa ugenini kuwavaa Tabora United, Septemba 11.

Timu hizo zinakutana ambapo Kagera Sugar haijaonja ladha ya ushindi msimu huu, huku Tabora United ikishinda mchezo mmoja dhidi ya Namungo kwa mabao 2-0 na kupoteza kwa Simba 4-0.

Chalamanda ambaye ni msimu wake wa nne kukipiga kikosini hapo, aliliambia Mwanaspoti kuwa licha ya kiwango walichoonyesha wachezaji, lakini yapo makosa waliyofanya na kujikuta wakiambulia patupu dakika 180.

Alisema alichobaini ni wachezaji kujisahau kwenye dakika za mwisho kwani mechi zote mabao waliyofungwa yalikuwa ya dakika za mwisho na kwamba wamelitambua hilo na kuanzia mchezo dhidi ya Tabora United wanataka kuonja alama tatu.

“Tumeona tulipokosea, nashukuru tumekuwa na maandalizi tangu mchezo dhidi ya Yanga na kwa sasa akili zetu zinawaza mechi ijayo na Tabora United ugenini na tunahitaji pointi tatu ili kujinasua chini,” alisema Chalamanda.

Kipa huyo aliongeza kuwa baada ya kuaminiwa kikosini katika mechi mbili za kwanza anahitaji kuonesha uwezo wake kuhakikisha anaendelea kulinda nafasi yake na kuendeleza kipaji chake akikiri kuwa vita ya namba ni kubwa.

Awali nyota huyo alikuwa anakabiliana na ushindani dhidi ya mpinzani wake kikosini Said Kipao, ambaye katika msimu uliopita alionekana kuaminiwa na sasa Chalamanda ameonesha kuwa chaguo la kwanza kwa benchi la ufundi na kazi yake imeonekana kuwa nzuri licha ya kupoteza michezo hiyo.

Related Posts