Mahakama kuamua iwapo basi la Kilimanjaro Express lipigwe mnada

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imepanga Septemba 11, 2024 kutoa uamuzi iwapo basi la Kilimanjaro Express kupigwa mnada au kuondoa mwenendo wa shauri la madai lililompa ushindi, Leonard Kisena kulipwa fidia ya Sh300 milioni baada ya basi hilo kusababisha kifo cha mtoto wa Kisena, Immaculate Kisena (16).

Uamuzi huo umetolewa leo Septemba 6, 2024 na Jaji Wilfred Dyansobera wa mahakama hiyo, baada ya kusikiliza maombi yaliyowasilishwa mahakamani hapo na mawakili wa Kampuni ya Kilimanjaro Truck Ltd na pingamizi zilizowasilishwa na Kisena kupinga maombi hayo ya kutaka shauri hilo lianze upya.

Jaji Dyansobera amesema maombi hayo yaliletwa chini ya hati ya dharura kwa hiyo pingamizi na maombi ya msingi atayasikiliza yote kwa pamoja.

Kampuni ya Kilimanjaro Truck Ltd kupitia wakili wake, Dickson Ngowi aliiomba Mahakama hiyo kutupilia mbali uamuzi wake iliyoyatoa Desemba 21, 2022 ambao kwa sasa upo kwenye utekelezaji.

Uamuzi huo ulimpa ushindi Kisena baada ya mahakama hiyo kuamuru kampuni hiyo kumlipa Kisena Sh300milioni ikiwa ni fidia kutokana na ajali ya basi hilo kusababisha kifo cha mtoto wa Kisena.

Ngowi alidai kuwa katika uendeshaji wa shauri hilo kuna taratibu za kisheria zilikosewa, hivyo aliomba mahakama ibariki shauri hilo lianze kusikilizwa upya.

Akijibu hoja hiyo, Wakili wa Kisena, Dk Aloys Rugazia akisaidiana na Valentine Charles amedai makosa ya kimwenendo hayawezi kukosolewa katika mahakama iliyofanya uamuzi.

Rugazia amedai badala yake waleta maombi walipaswa kukata rufaa kwa mujibu wa Sheria ya Madai (CPC), Kifungu cha 70 (2), lakini pia maombi hayo yaliwasilishwa mahakamani nje ya muda.

Wakili Rugazia amedai kabla ya usikilizwaji wa kesi hiyo, waleta maombi walipewa fursa ya kwenda kwenye usuluhishi lakini hawakutokea mara tatu ndipo jalada likarejeshwa kwa jaji Mgonya ili kesi iendelee ambapo pia hawakuwahi kufika mahakamani, hivyo haoni sababu ya shauri hilo kuanza upya.

Alidai kuwa mteja wake licha ya kupata madhara na kupoteza mtoto,  pia wadaiwa hawakuthamini ubinadamu, yaani kifo kilichotokea kwani baada ya ajali hiyo  hakuna mtu  kutoka katika kampuni hiyo aliyekwenda nyumbani wala kupiga simu kutoa pole.

Jaji Dyansobera baada ya kusikiliza hoja za pande mbili aliahirisha shauri hilo hadi Septemba 11, 2024 kwa ajili ya kutoa uamuzi juu ya maombi yaliyowasilishwa na waleta maombi na pamoja na majibu yaliyotolewa na wajibu maombi katika kesi hiyo ya madai.

Hata hivyo, wakati Jaji Dyansobera akitarajia kutoa uamuzi siku hiyo, tayari basi aina ya Scania lipo mikononi mwa dalali wa mahakama ambae ni Daniel Mbuga wa Legit Auction Mart, likitarajiwa kupigwa mnada Septemba 13, 2024.

Chimbuko la shauri hilo ni kesi ya madai namba 47/2022 iliyofunguliwa na Kisena mahakamani hapo akiomba alipwe Sh400 milioni na kampuni ya  Kilimanjaro Truck Company Limited, kama fidia baada ya basi lake kusababisha ajali iliyopoteza uhai wa mtoto wake mmoja.

Ajali hiyo ilitokea Desemba 24, 2021, eneo la Kerege wilayani Bagamoyo mkoani Pwani, wakati Kisena alipokuwa akisafiri na familia yake kwenda kwao Kilimanjaro kwa ajili ya kusherehekea Sikukuu za Krismas na Mwaka Mpya, akitumia gari lake binafsi.

Katika ajali hiyo, basi la Kilimanjaro aina ya Scania lenye namba za usajili T 278 ALQ lililokuwa liliacha njia na kuliparamia gari la Kisena aina ya Toyota Landcruiser lenye namba za usajili T.323 CWB.

Kufuatia ajali hiyo, mtoto wake mmoja wa kike aliyekuwa na umri wa miaka 16  alifariki dunia na Kisena, mkewe na mtoto wao mwingine wa kiume walinisurika japo walipata majeraha.

Hivyo dereva wa basi hilo, Mjahid Mohamed alifunguliwa kesi katika Mahakama ya Wilaya ya Bagamoyo akikabiliwa na mashtaka manne, yaani kuendesha gari lisilokuwa na bima, kusababisha kifo, kusababisha majeraha na kusababisha madhara ya uharibifu wa mali kwa kuendesha gari kwa uzembe.

Dereva huyo alikiri makosa hayo na Aprili 5, 2022, Hakimu Mwanakombo Mmanya alimtia hatiani na kumhukumu adhabu ya kulipia faini ya jumla ya Sh110, 000 kwa makosa yote au kifungo cha miezi Sita jela akishindwa kulipa faini hiyo.

Baada ya hukumu hiyo ndipo Kisena alipofungua kesi ya madai dhidi ya kampuni hiyo, Rowland Sawaya (Mkurugenzi mtendaji na mmiliki wa kampuni hiyo) na dereva wa basi hilo, Mjahid Mohamed.

Kisena alikuwa akidai fidia ya Sh400 milioni, ikijumuisha madhara ya jumla na ya hasara halisi kama vile  gharama za matengenezo ya gari lake lililoharibiwa , gharama za matibabu ya majeruhi na mazishi ya marehemu.

Kesi hiyo ilikuwa inasikilizwa na Jaji Leila Mgonya wa mahakama hiyo na baada ya kusikiliza kesi hiyo alitoa hukumu.

Katika hukumu yake jaji Mgonya, iliyosomwa Desemba 21, 2022 na Naibu Msajili Joseph Luambano, alikubaliana na hoja za upande wa madai na kuiamuru  Kampuni ya  Kilimanjaro Truck Company Limited, inayomiliki mabasi ya Kilimanjaro Express kumlipa Kisena  fidia ya Sh300milioni na riba ya asilimia saba kwa mwaka kuanzia tarehe ya hukumu mpaka kukamilisha malipo yote.

Hata hivyo tangu itolewe amri hiyo na mahakama, utekelezaji haukufanyika na Kisena kupitia wakili wake alirudi mahakamani kukazia hukumu hiyo.