Dodoma. Ni ukatili wa kutisha. Ndivyo unavyoweza kueleza mauaji ya Mwamvita Mwakibasi (33) na mwanaye Salma Ramadhan (13) yaliyotokea usiku wa kuamkia Septemba 6, 2024 Mtaa wa Muungano, Kata ya Mkonze jijini Dodoma, huku wahalifu hao ikielezwa walipakua wali na maharage kisha kwenda kula nyuma ya nyumba ya jirani.
Mwili wa mama ulikutwa kitandani, huku damu zikitoka shingoni ambapo inasadikika kuwa alichinjwa, huku Salma akikutwa chini karibu ya kitanda, akikoroma huku damu ikitoka puani na mwili haja kubwa ikimtoka.
Katika chumba hicho kilichoko karibu na sebule, ambacho ndicho walichokuwa wamelala Mwamvita, Salma na mdogo wake, kumetapakaa damu katika godoro na chini karibu na kitanda hicho.
Akizungumza leo Septemba 6, 2024 Mtaa wa Muungano, Kata ya Mkonze jijini Dodoma, mtoto wa kiume katika familia hiyo (jina limehifadhiwa), amesema mdogo wake (7), alimuamsha na kumweleza kuwa mama yake anavuja damu.
Amesema aliongozana na mdogo wake hadi katika chumba cha mama yake na kukuta akiwa anatoka damu katika maeneo mbalimbali ya mwili huku mdogo wake akiwa amelala chini.
“Alivyonipeleka chumbani nilikuta mama na mdogo wangu wakitoka damu, cha kufanya niliamua kutafuta simu ya mama na kumpigia mama mkubwa.
“Nimetafuta simu nikaikosa, nikachukua simu yangu, nilikuwa na namba ya bibi na ya babu tu. Nikampigia bibi anayeishi Mbeya nikamwambia ampigie mama mkubwa aje hapa nyumbani,”amesema.
Mtoto huyo amesema baada ya muda mama yake mkubwa Pendo Mwakibasi alikuja na marafiki zake na usafiri wakamchukua mama na mdogo wangu wakampeleka hospitali.
Alipoulizwa iwapo alisikia kelele zozote, usiku huo, mtoto huyo alisema kuwa hakusikia chochote hadi alipoamshwa na mdogo wake.
Amesema watu hao waliacha mlango ukiwa wazi na hivyo alipoamka aliufunga na kuwasubiri ndugu zake kumsaidia kumpeleka mama na mdogo wake hospitali.
Kwa upande wake, dada wa marehemu, Pendo Mwakibasi amesema alipigiwa simu na mama yake anayeishi Mkoa wa Mbeya saa 8.00 usiku wa kuamkia leo, akimtaka kwenda nyumbani kwa mdogo wake kwa sababu amevamiwa na watu wasiojulikana.
“Mama alinieleza nenda kwa mdogo wako Mwamvita kavamiwa, ikabidi nimwamshe jirani yangu na tulikuja wote hapa. Tulipofika tukakuta kweli amevamiwa na yupo pale kitandani akiwa ametapakaa damu, mtoto wake alikuwa amelala chini naye akiwa ametapakaa damu,” amesema.
Amesema aliwaita majirani ambao walimsaidia na kuwapeleka hospitali na kuwa mtoto mdogo (7) aliyekuwa akilala na mama yake ndiye aliyeanza kutambua mama na mdogo wake, baada ya kuamka ili mama yake ampeleke chooni lakini alishtuka kuona ametapakaa damu.
Amesema baada ya mtoto kumweleza kaka yake, alitafuta simu ya mama yake lakini hakuipata hivyo, aliamua kumpigia bibi yake aishiye Mkoa wa Mbeya ili aweze kumtafuta (Pendo).
Amesema wamemkuta Mwamvita akiwa amtapakaa damu sehemu za shingo, masikioni na puani huku mwili wa mtoto ukiwa chini umetapakaa damu.
“Inasemekana hao wahalifu walipakua chakula wali maharage wakaenda kula sehemu nyumba ya pili ambapo kumekutwa sahani na chakula kidogo.
Akizungumza na wananchi katika nyumba hiyo, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Dodoma, Daniel amewataka wakazi wa eneo hilo kuwa watulivu na kwamba Jeshi la Polisi linafanya uchunguzi juu ya tukio hilo.
“Ni tukio ambalo ni la kikatili kama tulivyoona mama wa watu alikuwa katika shughuli zake za kawaida na hadi jana usiku alikuwa na majirani katika sehemu ya kupumzika pale (kwenye duka lake). Kwa hiyo niwaombe wananchi muwe watulivu katika tukio hili,” amesema.
Amesema polisi wanaendelea na uchunguzi na kwamba wanaamini kuwa lazima wahusika watapatikana na kuchukuliwa hatua za kisheria, hivyo lisiwaletee taharuki.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Muungano katika Kata ya Mkonze, Yona Rubano amesema kuwa inasadikika watu hao walitumia ngazi kupanda ukuta wa nyumba katika sehemu ya barazani na kisha kushukia katika kochi kwa kutumia kamba.
“Nadhani miguu inaonekana hapo, baada ya kushuka walikuja moja kwa moja hadi katika chumba walichokuwa wakilala na watoto wake wa wawili. Baada ya kuja hapa wakaanza kuwaharibu na kuwafanyia unyama hauna maana ambao haujawahi kutolewa,”amesema.
Kaimu wa Kitengo cha Mahusiano na Uhusiano katika Hospitali ya Rufaa ya Dodoma, Lazaro Mbise alisema kuwa walipokea mwili wa Mwamvita saa 10 alfajiri ya leo akiwa amefariki dunia.