Sh100 milioni kurejesha maji Karatu

Karatu. Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema ndani ya siku saba Serikali itapeleka Sh100 milioni Karatu mkoani Arusha ili kurekebisha visima vilivyofunikwa na tope kutokana na mafuriko yaliyotokea Aprili 8, 2024.

Katika mafuriko hayo, Mtaa wa Mangafi ni miongoni mwa maeneo yaliyoathirika ambapo nyumba 502 zilifunikwa na maji, sambamba na kusababisha wananchi 7, 687 kukosa huduma ya maji baada ya visima kufunikwa.

Waziri Aweso ametoa ahadi mbele ya wananchi wa Karatu leo Ijumaa Septemba 6, 2024 baada ya kupigiwa simu na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla aliyekuwa anahutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Mazingira Bora.

Kabla ya kumpigia simu Aweso, Makalla amesema Serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha maji safi yanapatikana wilayani Karatu, lakini ghafla mafuriko yakatokea na kusababisha visima hivyo kuziba.

“Mheshimiwa Aweso nipo katika mkutano wa hadhara hapa Karatu, wananchi wana changamoto ya maji na mbunge wao ameomba hatua za dharura zichukuliwe ili maji yapatikane,” amesema Makalla.

Akijibu changamoto hiyo, Aweso aliwapata pole wananchi wa Karatu, akisema baada ya tukio wizara yake ilituma timu iliyofanya tathmini wilayani humo, lakini kutokana umuhimu wa visima hivyo, anamwelekeza katibu mkuu wake (Mwajuma Waziri) kutoa Sh100 milioni kwa ajili ya marekebisho ya visima hivyo.

Awali Mbunge wa Karatu (CCM), Daniel Awakii, alipaza sauti kuhusu hali hiayo akisema “tuna changamoto ya maji, tunaomba sauti yako maana mji wa Karatu ndiyo una shida wananchi hawa wana hamu ya kusikia sauti yako kuhusu suala hilo lililosababisha na maporomoko,” amesema.

Akutana na viongozi wa Ngorongoro

Baada ya mkutano wake kuzuiliwa na Jeshi ya Polisi kwa sababu za kiusalama, Makalla alitumia nafasi hiyo, kuonana na viongozi wa CCM na Serikali wa Ngorongoro na kufanya mazungumzo wilayani Karatu.

Hata hivyo, katika mazungumzo hayo Makalla hakuyaweka wazi badala yake aliutangazia umma kuwa CCM imesikiliza changamoto na ushauri wao, akiahidi kuupeleka ngazi ya juu ili ufanyiwe kazi.

“Kikao kilikuwa kirefu kwa masilahi ya wananchi wa Ngorongoro, wametueleza changamoto na njia za kuzipunguza, wametupa ushauri kama chama tumeupokea na tunakwenda kuufanyia kazi,” amesema Makalla.

Related Posts