Dar es Salaam. Mifumo ya kidijitali imeleta mafanikio katika kupunguza vifo vya mama na mtoto katika Hospitali ya Wilaya ya Kibaha, Tanzania.
Kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, Dk Wilford Kondo, kupitia mradi wa Afya-Tek, vifo vya mama na mtoto vimepungua kutoka saba kwa mwaka hadi kimoja tu mwaka 2024.
Mfumo huo wa kidijitali umeimarisha huduma za rufaa kwa kurahisisha usambazaji wa rekodi za afya kati ya vituo vya afya, jambo ambalo limeboresha uratibu wa huduma na kuokoa maisha.
Mradi huo pia unatoa elimu kwa vijana kuhusu afya ya akili, kuzuia mimba za utotoni, na magonjwa ya kuambukiza, hivyo kuimarisha afya ya vijana.
Mkuu wa Tehama wa Wizara ya Afya, Walter Disanjo, alieleza kuwa lengo ni kupeleka mfumo huo nchi nzima ili kuboresha huduma za afya kwa kila Mtanzania.
Mfumo huo pia umeboresha ukusanyaji wa data za afya na uratibu wa huduma, na sasa unasaidia kufanya maamuzi sahihi ya sera za afya.
Mkurugenzi wa Programu wa Apotheker Health Access Initiative, Dk Angel Dillip, ameongeza kuwa mfumo huu wa kidijitali umeondoa changamoto nyingi na kuleta urahisi katika utoaji wa huduma bora na haraka zaidi kwa wagonjwa.