Yanga Princess yaongeza kiungo Mnigeria

YANGA Princess imekamilisha usajili wa kiungo raia wa Nigeria, Adebisi Ameerat kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Hapoel Petach Tikva.

Mchezaji huyo ambaye ana uwezo wa kucheza kama kiungo mshambuliaji, kiungo mkabaji na pembeni, amesajiliwa akitokea Hapoel Petach Tikva ambayo inashiriki Ligi Kuu Israel.

Chanzo kimeliambia Mwanaspoti kuwa, tayari mchezaji huyo yupo nchini kwa ajili ya kuitumikia Yanga Princess na muda wowote anaweza kutangazwa.

“Alishasaini mkataba muda, lakini kuna baadhi ya vitu vilikuwa havijakamilika ndiyo maana alichelewa kutambulishwa, ila sasa mambo yako sawa,” kilisema chanzo hicho.

Msimu uliopita Yanga iliwapa mkono wa kwaheri wachezaji saba na tayari imetambulisha watatu ikiwa ni muda mfupi baada ya kumaliza msimu wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania (WPL), ikishika nafasi ya tatu kwa kukusanya pointi 36 kupitia mechi 18, huku Simba Queens ikitwaa ubingwa uliokuwa ukishikiliwa na JKT Queens iliyomaliza msimu ikiwa ya pili.