Zahera: Bado nipo nipo sana Namungo

BAADA ya tetesi nyingi kuhusiana na kocha Mwinyi Zahera kufanya makubaliano na uongozi kabla ya kupigtwa chini, mwenyewe ameibuka na kuweka wazi kuwa bado yupo sana Namungo.

Zahera ameiongoza timu hiyo katika mechi mbili za kwanza za Ligi Kuu Bara na kupoteza zote mbele ya Tabora United ilikalala 2-1 na Fountain Gate iliyowachapa 2-0 na hivyo kuzua taarifa kwamba alikuwa mbioni kupigwa chini kumfuata aliyekuwa Mtendaji Mkuu, Omary Kaya aliyejiuzulu mwenyewe.

Hata hivyo, Zahera aliliambia Mwanaspoti kwamba, uongozi ulichokifanya ni kumuongezea nguvu na sio kumtimua.

“Bado nipo na timu na naendelea kuinoa kama kawaida nikisaidiana na kocha msaidizi mpya waliyemuongeza kwenye benchi la ufundi Ngawina Ngawina,” alisema Zahera na kuongeza;

“Tumeanza vibaya ni sehemu ya matokeo nimekaa na viongozi tumezungumza na nimewaahidi kufanyia kazi upungufu ulioonekana na tutarudi tukiwa imara. Suala la mimi kuondolewa nimelisikia kama wewe tu lakini sina taarifa hiyo.”

Kocha huyo wa zamani wa Yanga, Polisi Tanzania na Coastal Union, alisema soka la Tanzania analifahamu vizuri na hatishwi na yanayosemwa, anapambana kuimarisha timu ili iweze kuwa kwenye ubora unaotakiwa huku akikiri kuwa kama wao wamepoteza nyumbani pia wanaweza kushinda ugenini.

“Ni mbaya kuanza na matokeo kama tuliyoanza nayo lakini haiondoi kuwa mpira una matokeo matatu kushinda, kufungwa na kupoteza hivyo mikakati inaendelea kuimarisha timu.”

Akizungumzia maandalizi kwa ujumla alisema wanaendelea vizuri kujiweka tayari kwa mchezo ujao dhidi ya Dodoma Jiji, utakaopigwa Septemba 12 kwenye Uwanja wa Tanzanite Manyara kutokana na Uwanja wa Jamhuri kufungwa kwa sasa kupisha marekebisho.

Related Posts