Kihenzile: Wanawake wa Kiislamu msichoke kusimamia maadili

Iringa. Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile ameliomba Baraza Kuu la Wanawake wa Kiislamu Tanzania, waendelee kusimamia maadili kwenye jamii ili kupambana na mmomonyoko unaoendelea kwa sasa.

Hata hivyo, amesema mpaka sasa wanawake hao wamefanikiwa kwenye malengo yao, hususani kupigania suala la mavazi ya kujisitiri.

Akizungumza leo Jumatatu Septemba 9, 2024 katika mkutano mkuu wa baraza hilo  unaofanyika katika Chuo cha Kiislamu, Iringa Mjini, Kihenzile ambaye pia mbunge wa Mufindi Kusini, alisema, “Mmeweza, hongera sana wanawake wa Kiislamu, kwanza mnajisitiri na mmekuwa mkihamasisha jamii. Nawaombea muendelee kusimamia maadili,” amesema Kihenzile.

Amesema Rais Samia Suluhu Hassan ni mfano mzuri wa malezi bora ya imani hiyo na kwamba wakiendelea kusimamia maadili watasaidia kupatikana kwa viongozi bora kwenye jamii.

“Lakini pia msisahau kutuombea wanaume, wanapitia changamoto na wana mzigo. Wakati mwingine wanalilia ndani kwenye moyo na nyie hamuwaoni. Msiwatenge,” amesema Kihenzile.

Ameliasa kundi hilo la wanawake kusaidia katika kukemea maovu yanayoendelea kufanyika kwenye jamii, ikiwamo ukatili wa kijinsia.

“Simamieni mtoto apate haki yake kwa sababu wanaofanya ukatili wapo hukohuko kwenye jamii,” amesema.

Awali, Naibu Katibu Mkuu wa Baraza la Wanawake wa Kiislamu Tanzania, Hawra Shamte amesema yapo mambo mengi wamefanikiwa tangu walipounda baraza hilo.

Amesema wamekuwa wakienda vijijini kutoa huduma kwa jamii, ikiwamo dawa na misaada mbalimbali kwenye jamii.

“Lengo letu ni kuwa wamoja na kushikamana, tunatembea vijijini kutoa mawaidha ya kuacha mabaya kwenye jamii na kutenda mema,” amesema Shamte.

Mpaka sasa baraza hilo lino wajumbe zaidi ya 3,000 nchi nzima. Walianza miaka 24 iliyopita wakiwa wanawake 100.