Hili ndilo linaloweza kuwa eneo maarufu zaidi katika Jiji la Dar es Salaam. Utasemaje kama unaijua Dar kama hujakanyaga mahala hapa penye soko kubwa zaidi nchini na pengine ukanda wa Afrika Mashariki?
Kariakoo licha ya umaarufu mkubwa utokanao na kuwa kitovu cha biashara kwa mkoa wa Dar es Salaam na Taifa kwa jumla, una historia ya kipekee. Na ndio maana makala haya yatakujuza japo kwa ufupi asili ya jina la eneo hili na kile kilichowahi kufanyika eneo hilo.
Historia inaonyesha jina hilo limetokana na maneno ya Kiingereza ‘Carrier corps’ yaani vikosi vya wabeba mizigo au wapagazi.Hawa walikuwa wabeba mizigo wakati wa vita ya kwanza ya dunia na eneo hilo likawa makazi ya kuanza na kufikia kwa misafara ya wapagazi hao waliokuwa wakisambaza kwa miguu vifaa kwa wanajeshi wa Kiingereza

Kwa kushindwa kutamka neno hilo, wenyeji wakafanya utohozi wakalipa jina la Kariakoo, jina lililoendelea kutumika mpaka sasa.
Kwa mujibu wa mwanahistoria bobezi wa habari za mji wa Dar es Salaam Alhaj Abadallah Tambaza, inawezekana pia neno Kariakoo kutokana na maneno Carrier call.
Hata hivyo, zipo simulizi kuwa eneo jina hilo pengine lilitokana na maneno ya Kiarabu Qaaria kullu yaani kijiji cha wote, na hivyo historia yake kuanza zamani zaidi kabla ya Waingereza kuja na kuanzisha kambi hiyo ya wapagazi.
Historia ya nyuma zaidi kabla ya mwaka 1900, inaonyesha eneo hilo lilikuwa kijiji kikubwa na shamba la minazi la aliyekuwa Sultan wa Zanzibar, Majid bin Said. Alikuwa na watumwa wengi wa Kiafrika eneo hilo.
Ujio wa utawala wa Mjerumani miaka ya 1880 ukaugawa mji wa Dar es Salaam katika kanda tatu ukiwatenga Wazungu walioishi maeneo jirani na ufukweni na Waafrika walioshi maeneo ya Kariakoo.

Huu ni mtaa wa Congo, mmoja wa mitaa maarufu kwa biashara katika eneo la Kariakoo.
Mwanzoni mwa miaka ya 1920, utawala huo ulijenga soko mahala ambapo leo kumesimama jengo kubwa lenye uhandisi uliotukuka chini ya mbunifu mhandisi mahiri, Beda Amuli aliyechora ramani ya Soko la sasa la Kariakoo lililoanza kujengwa mwaka 1970 na kukamilika 1974.
Akisimulia kuhusu soko la awali, Alhaj Tambaza anasema soko lenyewe lilikuwa limejengwa kwa mbao na kusimamishwa kwa vyuma na juu slimeezekwa mabati.
“Humo ndani sehemu za kufanyia biashara (vizimba) zilikuwa za mbao zilizojengwa kwa saruji na vikalio vya saruji pia. Katikati kulikuwa na njia ndogondogo za kutenganisha kati ya biashara na biashara, pamoja na watu kupita kwenda huku na kule,’’ anasimulia.
Alhaji Tambaza anasema, katika soko hilo, upande wa kaskazini kulikuwa na sehemu ya kuuzia samaki wabichi; waliokuwa wakiingia sokoni hapo kutokea maeneo ya Bagamoyo, Kunduchi, Msasani, Ununio na Mbweni.
“Mbele kidogo ya biashara ya samaki wabichi kulikuwa na eneo la wafanyabiashara ya samaki wakavu wa kuchoma au Waswahili waliwaita ‘samaki wa manyalia’ au wa kubanika,’’anasema.
Tumbaku, Ugoro biashara maarufu Kariakoo
Anasema, mbele ya mbao za samaki, kulikuwa na biashara ya tumbaku au ugoro, ambayo ilichukua eneno kubwa sana la soko.
Anasema, chumvi ya mawe na magadi ni biashara nyingine iliyokuwapo upande huo huku upande wa Magharibi mwa soko kwa ndani, ni sehemu iliyokuwa ya kuuzia bidhaa kama mihogo, viazi vitamu na magimbi.
Zipo simulizi kadhaa za kuvutia kuhusu eneo hili, lakini mojawapo ni kile kitendo cha watu kutoka maeneo mbalimbali ya mji kukusanyika hapo kwa minajili ya kusikiliza redio hasa taarifa ya habari.
” Sokoni kwa ndani ndimo mlikuwa na hiyo redio, nje kukawekwa spika watu wanakusanyika kusikiliza taarifa ya habari ya saa mbili usiku,” anasema Mzee Athumani Mwengeleko.
Unaweza kujiuliza kulikoni watu kukusanyika eneo hilo. Historia inaeleza kuwa wakati huo kituo cha redio kikiitwa Sauti ya Dar es Salaam, matangazo ya redio yalikuwa yakisikika maeneo ya Kariakoo, hiyo ikawa sababu wakazi kutoka viunga mbalimbali vya mji wakawa wanakusanyika hapo hususan kusikiliza taarifa za habari.

Sehemu ya chini ya Soko la Kariakoo maarufu kwa jina la shimoni. Picha kwa hisani ya Shirika la Masoko Kariakoo.
Hii ndio Kariakoo, kutoka shamba la minazi, kambi ya wapagazi na nyumba za udongo na nyasi, hadi leo ambapo eneo limejaa majengo ya kisasa, huku kila aina ya biashara ikifanyika hapo.
Leo Kariakoo ni kata katika Wilaya ya Ilala. kutoka soko la chakula na matunda, leo eneo hilo na viunga vyake limekuwa maarufu kwa aina nyingi za biashara.
Aidha, ndilo eneo lililo maskani ya timu kongwe za mpira wa miguu nchini kama vile Simba, Yanga, Pan African, Cosmopolitan na nyinginezo.
Kuna mengi kuhusu eneo hili ambayo makala haya hayajaangazia. Pengine watafiti wengine watafukua zaidi historia sahihi ya Kariakoo kwa kumbukumbu ya vizazi vijavyo.

Mwonekano wa mtaa mmojawapo wa Kariakoo miaka ya 1950.