Simiyu. Wakati mabadiliko ya tabianchi yakizidi kushika kasi duniani, Jamii ya kabila la Wahadzabe wanaoishi katika mapori yaliyopo Meatu mkoani Simiyu, imekabidhiwa mradi wa ufugaji wa ndege pori ili kupambana na uwindaji haramu na kuimarisha ustawi wa kaya zao.
Wahadzabe ni kabila linaloishi msituni katika maeneo mbalimbali nchini, huku likitegemea shughuli za uwindaji na ukusanyaji matunda kuishi.
Mradi huo uliofadhiriwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) chini ya mwamvuli wa Asasi ya Afrinurture For Peoples’ Development (Afripedo), unaotekelezwa kwa awamu tatu kwa gharama ya zaidi ya Sh228 milioni (Dola 84,000 za Marekani). Unatekelezwa kuanzia Septemba 2024 hadi Septemba 2025.
Akizundua mradi huo leo Jumatatu Septemba 9, 2024, Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Faudhia Ngatumbura amesema si tu utasaidia upatikanaji wa chakula na kipato kwa kaya za kabila hilo, pia kutasaidia kwenye uhifadhi wa mazingira na utaendeleza mila na desturi za kabila hilo.
“Mradi huu unakwenda kutoa suluhisho la kupata kitoweo kwa kabila la Wahazabe, niwaombeni tuupokee huu mradi, tuutunze ili kufikia malengo yaliyotarajiwa, ikiwemo kitoweo katika familia zetu tukifanya hivyo tutapunguza tatizo la uhaba wa kitoweo kwa jamii yetu ya Kihadzabe,” amesema Ngatumbura.
Amesema uzoefu unaonyesha Wahadzabe ni miongoni mwa makabila yanayopitia changamoto kutokana na mabadiliko ya tabianchi na kushamiri kwa shughuli za kibinadamu nchini.
“Jamii hii ina changamoto kama mlivyosema kwenye risala yenu na ukiangalia historia yenu mlianzia Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga na mmekuwa mkisogea kila siku na kwenda meneo ya pembezoni, hili eneo lenu ni la asili mnawajibu wa kutunza mazingira na kulifanya kuwa eneo lenu la makazi ya kudumu,” amesema.
Mratibu wa mradi huo kutoka Asasi ya Kiraia ya Afripedo, Revocatus Meney amesema kuanzishwa kwa shamba hilo la ufugaji wa ndege pori lenye ukubwa wa ekari 21 katika Kijiji cha Makao unatarajia kunufaisha Wahadzabe zaidi ya 1,300 wanaoishi wilayani Meatu.
“Haya ni matokeo ya jitihada za Serikali Taasisi ya Usimamizi wa Wanyamapori nchini (Tawa) iliyokuja na kanuni ya kuanzisha mashamba ya kufuga wanyamapori (Wildlife Conservation Management of Wildlife Captive Facilities) ya mwaka 2020. Hii itapanua wigo kwa kutoa ruhusa ya kufuga na kunufaika na wanyamapori,” amesema.
Amesema kupitia mradi huo utatumika kama shamba darasa kwa jamii inayoishi kuzunguka eneo hilo, ili kutoa fursa kwa wananchi wengine kujifunza kuhusiana na ufugaji wanyamapori.
Ametaja aina ya ndege watakaofugwa katika shamba hilo linalogusa Kijiji cha Makao na Sungu kuwa ni pamoja na kuku wa kienyeji, bata mzinga, maladi, pekini na huku ndege pori wanaofungwa humo kuwa ni kanga, mbuni, tandawala wakubwa, bata bukini, taji (korongo – taji) na bata domokifundo.
Kwa upande wake, Mkazi wa Kijiji cha Sungu wilayani humo, Jape Jape amesema baada ya kuanza utekelezaji wa mradi huo huenda ukapunguza ama kuondoa baadhi ya vitendo, ikiwemo vya uwindaji haramu wa wanyamapori katika mbuga na mapori tengefu wilayani humo.
“Awali tulikuwa tukiingia porini na kuwinda wanyama kwa ajili ya kitoweo, sasa kwa kufuga tutapata kitoweo chetu kwa njia halali kuliko ile ya zamani ambapo tulikuwa tukiingia porini na kuanza kuwinda wanyama kwa kutumia silaha zetu za jadi,” amesema Jape.
Naye Martha Shimba amesema uamuzi wa kuanzisha shamba hilo utasaidia wanawake wa jamii ya Wahadzabe kutotumia muda mwingi katika utafutaji wa wanyamapori, badala yake watawekeza kwenye shughuli za uzalishaji mali na kuangalia familia zao.