Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Julius Nyerere (MNF), Joseph Butiku amewataka viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama wasiseme hawawajui wahusika wa uhalifu kwa kuwa wanaishi kwenye jamii.
Sambamba na hilo, Butiku ametaka uwajibikaji wa viongozi inapotokea maeneo waliyopewa kuyaongoza yameingia doa kwa namna yoyote.
Kauli hiyo ya Butiku, inakuja katika kipindi ambacho kumekuwa na mfululizo wa taarifa za matukio ya utekaji na mauaji ya raia na taarifa ya Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), iliorodheshesha watu 83 waliokumbwa na kadhia hizo.
Hata hivyo, kauli ya kiongozi huyo wa zamani serikalini, inakoleza matamko ya wadau hasa baada ya tukio la kutekwa na kuuawa kwa kada wa Chadema, Ali Kibao.
Kibao alitekwa na watu wasiojulikana jioni ya Septemba 6, 2024, eneo la Kibo Complex, Tegeta jijini Dar es Salaam akiwa ndani ya basi la Tashriff akielekea nyumbani kwake, mkoani Tanga.
Mwili wa Kibao uliokutwa Ununio, Dar es Salaam na mwili wake ulizikwa jana Jumatatu, Kijiji cha cha Tarigube kata ya Togoni, Tanga.
Tukio hilo la Kibao lililaaniwa na Rais Samia Suluhu Hassan akieleza kufanywa kwa uchunguzi na kupelekewa taarifa haraka.
“Nimeagiza vyombo vya uchunguzi kuniletea taarifa ya kina kuhusu tukio hili baya kabisa na mengine ya namna hii haraka. Nchi yetu ni ya kidemokrasia na kila raia ana haki ya kuishi.
“Serikali ninayoiongoza haivumilii vitendo vya kikatili vya namna hii,” aliandika Rais Samia katika mitandao yake hiyo.
Leo Jumanne, Septemba 10, 2024, Butiku amezungumza na waandishi wa habari, katika ofisi za taasisi hiyo, Posta jijini Dar es Salaam.
“Wasitwambie hawajui, lazima wajue laa sivyo hawana sababu ya kuwa pale,” amesema.
Butiku amesema lazima Serikali iwajue kwa sababu wanaishi miongoni mwa wananchi, katika kaya, wapo ndani ya vyombo vya dola, wapo makanisani na katika misikiti.
“Huwezi kuwa waziri, halafu watu wanatekwa na kuuawa kisha unasema Rais ameagiza, Rais kazi yake ni kupewa taarifa ili aagize, wajibu wa kwanza kwenye matukio haya ni wako wewe.
“Ukipewa kundi uliongoze, mambo ya aibu yakitokea katika kundi lile, nani unamuuliza. Tunachosema kuhusu vyombo vya ulinzi na usalama sio wote, hatutaki kuwalaumu wote,” amesema.
Butiku amesema Watanzania wanapaswa kuelewa kuwa Tanzania sio Taifa la wauaji wala wahuni ni la watu wanaoishi kwa kuzingatia Katiba na sheria.
Amewataka wananchi kumsaidia Rais kuwapata wabaya ili wachukuliwe hatua kwa kuwa mkuu huyo wa nchi ana vyombo vya dola vyenye utaalamu.
“Tanzania ina Rais mmoja aliyekabidhiwa Katiba aitumie kuiongoza nchi na kulinda Taifa na mali zake, anapaswa kuungwa mkono bila kusita na katika hilo bila maswali,” amesema.