Dar es Salaam. Watu watano akiwamo bibi wa miaka 70, Felista Mwanri na mwanawe Richard Mwanri (47) wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakabiliwa na shtaka la kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi zenye uzito wa zaidi ya tani moja.
Washtakiwa wengine ni Athuman Mohamed, maarufu Makame (58) mkazi wa Tanga, Juma Chappa (36), mkazi wa Kiwalani na Omary Mohamed (32) ambaye ni dereva na Mkazi wa Buza, Dar es Salaam.
Kabla ya kusomewa shtaka hilo, leo Jumanne, Septemba 10, 2024 Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakaka hiyo, Godfrey Mhini amesema washtakiwa hao hawatakiwi kujibu chochote kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za dawa za kulevya.
Pia, Hakimu Mhini amesema shtaka linalowakabili washtakiwa hao halina dhamana hivyo, wataendelea kubaki rumande.
Baada ya kueleza hayo, Wakili wa Serikali, Eric Davis amewasomea shtaka la kusafirisha dawa za kulevya kinyume cha sheria.
Amedai kwa pamoja wanadaiwa kutenda kosa hilo, Agosti 28, 2024 eneo la Tairo Luguruni Barabara ya Kwembe ndani ya Wilaya ya Ubungo.
Siku hiyo ya tukio, washtakiwa kwa pamoja walikutwa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya bangi zenye uzito wa kilo 1815, kinyume cha sheria.
Davis baada ya kuwasomewa shtaka hilo amedai upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika na wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Hakimu Mhini ameahirisha kesi hiyo hadi Septemba 24, 2024 itakapoitwa kwa ajili ya kutajwa na kuangalia hatua ya upelelezi ilipofikia.
Washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na shtaka linalowakabili halina dhamana.