TIMU ya Young Profile imeifunga Crossover kwa pointi 52-49 katika Ligi ya Kikapu Mwanza kwenye mchezo uliofanyika katika Uwanja wa Mirongo mjini humo.
Ushindi wa Young Profile ulitokana na muda wa nyongeza ulioongezwa baada ya timu hizo kufungana pointi 43-43 katika robo zote nne.
Baada ya dakika tano kuongezwa, Young Profile ilianza mchezo kwa kasi huku ikitumia makosa ya Crossover kupoteza mipira yao maarufu kama turn over.
Katika mchezo huo nyota wa Young Profile maarufu kama Hamisi alifunga pointi 14 na aliongoza pia kwa kudaka mipira ya rebound akifanya hivyo mara tano.
Katika mchezo mwingine uliochezwa uwanjani hapo, Eagle ilizinduka baada ya kuifunga Sengerema Hoopers kwa pointi 52-49. Lubango wa Eagle aliongoza kwa kufunga pointi 15 na kuasisti mata tano.
Eagle katika michezo iliyocheza ilifungwa na Planet mara mbili kwa pointi 62-59 na 81-72. Timu zinazoshiriki katika ligi hiyo ni Sengerema Hoopers, CUHAS, Oratorio, Profile, Young Profile, Mwanza Eagles, Planet na CIC.