SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) chini ya Rais Wallace Karia, limetekeleza ahadi liliyoitoa wikiendi iliyopita kwa mshambuliaji wa zamani wa Polisi Tanzania, Gerald Mdamu kumlipia gharama za matibabu, ambapo nyota huyo ni kama ameanza maisha mapya baada ya mateso ya zaidi ya miaka miwili.
Julai 9, mwaka 2021, basi la Polisi Tanzania lilipata ajali likitoka katika mazoezi kwenye Uwanja wa TPC mjini Moshi kwenda kambini, ambapo Mdamu alivunjika miguu yote na baada ya ajali alitibiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, lakini hakupona vizuri na sasa ameanza tena matibabu TFF ikijitosa kumgharimia ukiwa ni mwanzo wa maisha mapya yenye matumaini.
Gerard Mdamu kabla ya kupata majeraha yanayomtesa kwa sasa
Daktari bingwa wa magonjwa ya mifupa wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (Moi), Kennedy Nchimbi, aliyemfanyia upasuaji mara ya mwisho ndiye aliyemfanyia tathimini ya matibabu yake mapya yaliyokuwa yanahitaji Sh 1.5 milioni.
Kiasi hicho cha pesa kimelipwa na TFF moja kwa moja Moi, na jana Jumatano Mdamu alianza kwa kupigwa X ray ili kuonyesha tatizo kabla ya kuendelea na matibabu ikiwa ni siku chache baada ya Mwanaspoti kuripoti hali aliyonayo akiomba msaada kwa wadau.
Akizungumza leo, Mdamu alisema ameanza matibabu na ndani ya siku mbili zijazo huenda akapigiwa simu ili kwenda kufanyiwa upasuaji.
Wadau wengine waliojitoa kuhakikisha afya ya mchezaji huyo inatengemaa ni makamu wa rais wa Yanga, Arafat Haji aliyetoa Sh 1.5 milioni, Mwamnyeto Foundation iliyopo chini ya nahodha wa Yanga, Bakari Mwamnyeto na kiungo wa Singida Big Stars, Zawadi Mauya walitoa Sh 1.5 milioni, pia na Watanzania mbalimbali ambao wanaendelea kutuma kupitia ‘lipa namba’.
Kabla ya kuanza matibabu Mdamu alikuwa amefikia hatua ya kukata tamaa kutokana na kutokuwa na uwezo.